Chanzo makini kimeliambia gazeti hili kwamba, Kajala ambaye alitoka mahabusu ya Segerea jijini Dar, Machi 25, 2013 akiwa hana mbele wala nyuma kiasi cha kutia huruma, sasa anazikamata za kutosha kiasi cha watu wake wa karibu kumshangaa.
MANUNUZI YAKE
Chanzo kimebainisha kuwa, Kajala ameagiza kutoka China kontena lenye urefu wa futi 20 likiwa limesheheni samani za ndani. Samani za ndani ni fenicha mbalimbali.
“Hivi mnajua kwamba Kajala yuko juu. Naweza kusema ni tajiri kwa sasa, maisha yake ni poa. Hivi ninavyoongea kuna kontena la futi arobaini linakuja Dar, ndani mna samani tu,” kilisema chanzo hicho.
AMWAGA MILIONI 90 KUTENGENEZA FILAMU
Katika hali inayoendelea kutafsiriwa kuwa ni kuzidi kuonesha ukwasi alionao, msanii huyo ameshatumia shilingi milioni 90 kwa ajili ya kutengeneza filamu zake tatu, kila moja ikitumia bajeti ya milioni 30 za Kibongo.
Filamu ya Kajala ambayo iko njiani kutoka inaitwa Laana. Inadaiwa mpango wake ni kutengeneza filamu 10 ambazo atakuwa akiziuza kwa nyodo. Kama ni hivyo atatumia shilingi milioni 300 kwa filamu hizo kumi.
ATUMIA MILIONI 11 KUNUNUA VITO VYA THAMANI
Mbali na kuvaa magauni na viatu vya bei mbaya, hivi karibu staa huyo alitua Dar akitokea China ambapo alipigilia vito vya gharama ya maisha ya familia nzima.
“Juzikati Kajala katoka China na cheni ya dhahabu kainunua dola za Marekani elfu tatu, bangiri pia ya dhahabu ya dola elfu mbili na mia tano na hereni za gold (dhahabu) za dola elfu moja mia tano,” kilisema chanzo.
Kwa mahesabu ya sasa, kiasi hicho cha dola kikibadilishwa na shilingi ya Tanzania, Kajala alitumia kama milioni 11 kununua vito hivyo tu.
ANAYEMPA JEURI ATAJWA
Inadaiwa mcheza filamu huyo amekuwa akipata jeuri hiyo kutoka kwa mwanaume bilionea wa Ghana aliyejulikana kwa jina moja la Safara ambaye walikutana nchini China. Inadaiwa Safara anaishi Marekani lakini ndiye anayeshika tenda ya kuinunulia serikali ya Ghana vitu mbalimbali.
MWISHO DESEMBA KUISHI NYUMBA YA KUPANGA
Habari zikazidi kumiminika kwamba, Safara amemwambia Kajala mwisho Desemba mwaka huu kuishi kwenye nyumba ya kupanga, mwakani mjengo wake utakuwa umekamilika.
Hata hivyo, haijaelezwa kama ameshapata kiwanja cha kujengea au la! Ingawa habari zinasema nyumba anayoishi sasa Kajala imeshalipiwa kodi ya mwaka mmoja na tajiri huyo wa Ghana.
AMFADHILI WEMA
Ikazidi kudaiwa kuwa, katika ziara ya baadhi ya mastaa jijini Arusha hivi karibuni wakiongozwa na Wema ambako kulikuwa na shoo ya muziki wa Kizazi Kipya, Kajala alimsaidia Wema mambo mbalimbali zikiwemo pesa ili kufanikisha shughuli hiyo iliyohitaji umakini wa hali ya juu.
“Mbali na fedha hizo, Kajala wa zamani si huyu wa sasa, ila ninashomsifu bado anamheshimu sana Wema, anajua ndiye amechangia mafanikio yake, kama siku zile asingetoa zile milioni kumi na tatu Kajala angekuwa gerezani,” kilisema chanzo hicho.
ALIPOTOKA GEREZANI
Inadaiwa baada ya kutoka Segerea, Kajala aliishi maisha ya kuwa na shida hata shilingi elfu kumi ilimsumbua, Wema ndiye aliyekuwa akimbeba kwa vijisenti vya matumizi na baadaye alimwajiri kwenye kampuni yake ya filamu ya Endless Fame kama sekretari. Kampuni hiyo kwa sasa imesimama.
HUENDA CHINA KINYEMELA?
Baada ya kuona safari zake zimezaa matunda na kuhisi watu wanafuatilia nyendo zake, likiwemo gazeti hili, Kajala ambaye husafiri mara kwa mara, amekuwa akidai anakwenda Zanzibar licha ya hati zake za kusafiria kuoneshwa zimegongwa mihuri ya China na Dubai.
KAJALA SASA
Alipoulizwa kwa njia ya simu juzi kuhusiana na ukwasi wake kwa sasa, Kajala alisema anachojua yeye anaishi maisha ya kawaida, tafsiri kwamba amekuwa tajiri ghafla inafanywa na watu wanaomuona.
“Mimi naishi kawaida tu, huo utajiri wanauona wao. Unajua haya ni maisha, leo unakuwa hivi, kesho unakuwa vile ndicho ninachoweza kukisema, siwezi kusimulia kila kitu,” Alisema kajala
No comments:
Post a Comment