1. Utangulizi
Katika kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe 20 - 22 Novemba
2013, Kamati Kuu ya CHADEMA, pamoja na mambo mengine, iliazimia kunivua
nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama.
Kwa mujibu wa taarifa ya
chama iliyotolewa katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa
tarehe 22 Novemba 2013, ilielezwa kwamba sababu za kuvuliwa uongozi mimi
na Dk Kitila Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na waraka
unaojulikana kama mkakati wa uchaguzi 2013.
Ukweli ni kwamba waraka
uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama
ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu . Sababu za kufukuzwa kwangu
kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ni tuhuma lukuki ambazo
si mara yangu ya kwanza kuzisikia zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya
chama.
Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi nimekuwa nikikisaliti
chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa. Nitazianisha tuhuma hizi
na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali
vyama.
Ninatambua kwamba chama changu kinapita katika wakati mgumu sana sasa
hivi. Nataka nitamke mapema sana kwamba mimi Zitto Zuberi Kabwe sitokuwa
chanzo cha CHADEMA kuvunjika.
Hiki ndicho chama kilichonilea na
kunifikisha hivi nilivyo. Ningependa chama hiki mtoto wangu atakapokuwa
mtu mzima na atakapoamua kujiunga na siasa aingie CHADEMA.
Bado nina
imani kubwa na chama changu na ninaamini ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana, leo na kesho.
2. Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu
Zipo tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya
chama na nje ya vikao na baadhi ya viongozi wenzangu.
Tuhuma hizi
zinalenga kuonyesha kwamba mimi ni mbinafsi na kwamba ninapokea rushwa
ili kukihujumu chama changu.
Nitazianisha tuhuma kwa kifupi na kuzijibu
kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama.
i) Tuhuma kwamba sikushiriki kumpigia kampeni mgombea wetu wa urais
katika uchaguzi wa mwaka 2010. Ningependa kueleza yafuatayo kuhusu jambo
hili:
- Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kaskazini huko Kigoma.
- Pamoja
na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika majimbo mengine 16
katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Pwani,
Shinyanga, Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya
kampeni katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais.
- Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na Rais.
- Katika
Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais katika kata zote za Kigoma
Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.
ii) Tuhuma kwamba katika Mkoa wa Kigoma nilishindwa kuwapigia kampeni
wagombea wetu kiasi kwamba peke yangu ndiye niliyeshinda katika uchaguzi
huo. Ukweli ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu, na hivyo
ndivyo wapiga kura wa Kigoma walivyoamua.
iii) Tuhuma kwamba nilishiriki kuwashawishi wagombea wetu katika baadhi
ya majimbo kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea
wa CCM wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa. Majimbo yanayotajwa ni
pamoja na Sumbawanga, Musoma Vijijini na Singida Mjini.
Kama
nilivyokwisha kueleza katika vikao mbalimbali vya chama jambo hili si la
kweli na hakuna popote ambapo watoa tuhuma hizi wamewahi kutoa ushahidi
kwamba nilifanya jambo hili.
Nipo tayari kwa uchunguzi ndani ya chama
na watoa tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama
kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila
uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho.
iv) Tuhuma kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni mbalimbali za
chama: Ukweli ni kwamba nimeshiriki sana katika operesheni mbalimbali za
chama ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na
operesheni kubwa katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na
nilikwenda katika mikoa yote tuliyotembelea.
Mwaka 2012 baada ya hoja ya
mkonge bungeni nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka 2012 kulikuwa na
operesheni kubwa moja katika mikoa ya kusini ya Mtwara na Lindi.
Operesheni hii sikushiriki kwa sababu nilikuwa nchini Marekani kufungua
matawi kwa mwaliko wa Watanzania wanaoishi huko.
v) Tuhuma kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba
Hesabu za Vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG): Katika jambo hili ninatuhumiwa kwamba mimi kama Naibu
Katibu nilipaswa kuwasiliana kwanza na viongozi wa chama 'kuwatonya'
ili wajiandae.
Kwamba kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka
kundi moja na CCM na nastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa
yangu nilikuwa na nia mbaya na chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa
na ambayo ningependa kuyakariri hapa kuhusu jambo hili ni kama
ifuatavyo:
- Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya
uenyekiti wa PAC kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya
hivyo ni kuendeleza tabia zile zile ambazo tunazipinga na ambazo
tunapigania kuzibadilisha
- Napenda kusisitiza kwamba
hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Serikali (CAG). Natambua kwamba mahesabu ya chama changu yamekuwa
yakikaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu tuliojiwekea. Lakini
matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa hayajakaguliwa
na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa hili ni la nani.
vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu kuchukua Posho za Vikao
Mtakumbuka kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011 kama
ishara ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa kupinga posho
za kukaa na matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama
ilivyoanishwa kwenye Ilani yetu ya mwaka 2010-2015. Mtakumbuka kwamba
hivi karibuni Mheshimiwa Lema amenishutumu kwamba kukataa kwangu
kuchukua posho ni unafiki kwa sababu ninapokea posho kubwa zaidi katika
mashirika ya umma ambapo mimi ni mwenyekiti wa kamati husika. Ninapenda
kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:
- Sipokei posho yeyote ya vikao (sitting allowance) ndani
na nje ya Bunge tangu mwaka 2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika
Kamati za Bunge ninavyohudhuria. Mtu yeyote mwenye ushahidi vinginevyo
auweke hadharani.
- Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la kiilani katika chama chetu, na kwangu ni swala la kimisingi
zaidi. Katika Wilaya yangu vifo vya kina mama wajawazito ni 1900 kati
ya wanawake 100,000 wenye ujauzito. Vifo hivi vinatokana na ukosefu wa
huduma kwa sababu ya bajeti finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa chama
chetu kuliweka swala la kupunguza matumizi ya Serikali katika Ilani, na
kuondoa posho za wabunge, ambao tayari wanapokea mishahara mikubwa,
kungesaidia sana kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina
mama.
- Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa Lema. Ni suala la msingi katika chama chetu.
3. Usambazaji wa Ripoti ya Siri kuhusu Zitto Kabwe
Hivi karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya siri kuhusu mimi
ukibeba lundo la tuhuma kwamba nimehongwa fedha nyingi ili kukihujumu
chama changu. Waraka huu ulidaiwa kuwa umechomolewa kutoka makao makuu
ya CHADEMA.
Jambo hili pia lilijadiliwa katika kikao cha juzi kwa
kifupi, na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni kwamba waraka huu
haukuandaliwa wala kusambazwa na makao makuu. Katika mchango wangu
nililalamikia mambo matatu yafuatayo:
- Kwamba baadhi ya waliokuwa wanasambaza
waraka ule walikuwa ni viongozi wa chama chetu. Bahati mbaya hadi leo
hakuna hata mmoja ambaye amekwishachukuliwa hatua za kinidhamu.
Ninaamini kwamba kuna siku watu hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa
taratibu za chama chetu.
- Kwa kuwa chama kimekana rasmi
kuhusika na waraka huu, nitaendelea na taratibu za kisheria ili
kuhakikisha kwamba wote waliohusika kutengeneza hekaya ile wanachukuliwa
hatua stahiki za kisheria.
4. Hitimisho
Ninatambua kwamba kuna watu walitegemea leo ningejibu mapigo na
ningewazodoa watu kwa majina kama ilivyo kawaida katika siasa za
Tanzania.
Natambua pia kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro
katika vyama vya siasa hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo
ningetangaza 'maamuzi magumu'.
Natambua kwamba wapo ambao wangependa
kupata nafasi ya kuendelea kutumia suala hili katika harakati zao za
kudhoofisha mapambano ya demokrasia na uthabiti wa siasa za ushindani
nchini mwetu.
Napenda wanachama wa CHADEMA na wapenda demokrasia na siasa safi wote nchini watambue
kwamba mimi bado ni mwanachama mwaminifu wa chama hiki na nitakuwa wa
mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari yangu. Nitafuata taratibu zote
ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.
Naomba wanachama waelewe kwamba mimi kama binadamu ninaumia ninapopigwa.
Tuhuma ninazorushiwa ni kubwa na zinanikwaza. Tuache siasa za uzushi
ili tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe Watanzania
wenye matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.
Kama mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa muda sasa yapo
mengi mazuri nimeyafanya. Lakini kuna maeneo nilipojikwaa na yapo makosa
niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya siasa.
Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia.
Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina, waumini
wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya
watukuzao siasa majitaka.
Hii ni changamoto kubwa ndani ya chama chetu
inayohitaji uongozi shupavu kuikabili. Nitasimama daima upande wa
demokrasia.
Kama alivyopata kunena mmoja ya wanasiasa maarufu, 'kiwango
cha juu kabisa cha uzalendo katika nchi ni kukubali kutofautiana
kimawazo', na ninatamani huu ndio uwe utamaduni wa chama chetu.
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Dar es Salaam.
24 Novemba, 2013