Monday 25 November 2013

CHUJI, CANNAVARO, MSUVA NA JERRY TEGETE WAONGEZA MIKATABA YANGA - KUBAKI JANGWANI MPAKA 2016


Wachezaji watano wa timu ya Young Africans wameongeza mikataba ya muda mrefu ambapo sasa wataendelea kuitumikia klabu yenye maskani yake mitaa ya Twiga/Jangwani mpaka mwaka 2016, hili limefanywa na uongozi kwa mapendekezo ya benchi la ufundi.

Wachezaji ambao mpaka sasa wameshaongeza mikataba ya kuitumikia klabu ya Young Africans ni walinzi Kelvin Yondani (2014-2016), Nadir Haroub "Cannavaro" (2014-2016), kiungo Athuman Idd (2014-2016), mshambuliaji Saimon Msuva (2014-2016) na Jerson Tegete (2014-2016).

Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu ya Young Africans Abdallah Bin Kleb amesema hao ni baadhi tu ya wachezaji ambao wameshamaliza taratibu zote na kusaini mikataba mipya itakayowafanya waitumikie Yanga mpaka mwaka 2016.

"Tupo katika mazungumzo ya mwisho na wachezaji wetu wengine, mazungumzo yanaendelea vizuri na tunaamini muda si mrefu nao tutakua tumeshamalizana nao ili waweze kuendelea kuitumika Yanga tena kwa muda mrefu "alisema Bin Kleb.

Wakati huo huo kikosi cha Young Africans leo kimeanza mazoezi asubuhi katika uwanja wa Bora - Mabatini Kijitonyama kujiandaa na mchezo wa hisani dhidi ya Simba SC Disemba 14, 2013, mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.


No comments:

Post a Comment