Wednesday 29 January 2014

BUNGE LATAKA MGOGOLO BUKOBA UISHE

                      Mh  Benadetha Mshashu

MAKAMU Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Benadetha Mshashu, ameitaka wizara husika kuhakikisha inasimamia na kuupatia ufumbuzi mgogoro wa uongozi katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.
Hatua hiyo inakuja zikiwa ni siku chache tangu aliyekuwa Meya wa manispaa hiyo, Anatory Amani, kutengua msimamo wake wa kujiuzulu baada ya taarifa ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kumtia hatiani kwa ubadhirifu wa miradi ya maendeleo aliyokuwa akiitekeleza.
Akizungumza jana wakati kamati hiyo ilipokutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia, Benadetha alisema Bukoba inafuka moshi, hivyo ni vyema wizara hiyo ikasimamia sheria ili kuinusuru halmashauri ifanye kazi.
Alisema kuwa halmashauri hiyo ni vyema ikanusuriwa ili itende kazi kwani baada ya ripoti ya CAG kutoka nakala zake zimegawiwa hadi mitaani.
Akijibu hoja hiyo Waziri Ghasia, alisema kuwa walishakutana na kuamua kuwa meya wa manispaa hiyo ajiuzulu ama madiwani wapige kura za kumuondoa au Baraza la Madiwani livunjwe na kueleza kuwa atalifanyia kazi suala hilo.
Katika hatua nyingine, Ghasia alijitetea kuwa anaitwa waziri mzigo kwa sababu Tamisemi haina meno ya kuwashughulikia watendaji kutokana na sheria za nchi zilizopo.
Ghasia alisema kuwa Baraza la Madiwani wakishindwa kuwachukulia hatua watendaji, Waziri wa Tamisemi hawezi kuchukua hatua kutokana na sheria zilizopo bali wakurugenzi wanachukuliwa hatua na Waziri Mkuu.
Suala la mawaziri mizigo lilijitokeza jana baada ya Mwenyekiti wa kamati hiyo Dk. Khamis Kigwangalah, kueleza kuwa mfumo wa sheria katika kuwachukulia hatua za kinidhamu wakurugenzi ni tatizo.
“Sheria ya Utumishi wa Umma namba 8 ya mwaka 2002 haiko sawa, ikiwezekana ijadiliwe upya, maana kila mtu kilio ni halmashauri, mawaziri wameambiwa mizigo, kombora zimepigwa kwao, madaraka waliyopewa madiwani, wakurugenzi hawawasilikizi, wananchi wamepewa mamlaka ya kiujanja ujanja tu ya kuwashughulikia wakurugenzi. Mfumo ni tatizo.
“Ziangaliwe upya sheria kama madiwani hawawezi kuwasimamia, madaraka yapunguzwe na kama mfumo huu wa sasa wa uendeshaji wa halmashauri utaendelea nyie mawaziri mtaendelea kushambuliwa tu, maana usiri wa halmashauri unasababisha urahisi wa kuiba,” alisema.
Katika maazimio yake, kamati hiyo ilitaka kikao hicho kihairishwe kwa wiki mbili ili wizara hiyo iwape majibu ya kina ya hoja zilizowakilishwa zitolewe kwa maandishi ikiwemo watu wa hazina wawepo, mtindo wa ripoti uonyeshe bajeti ni kiasi gani, kilichotolewa na asilimia ionekane.
Maazimio mengine ni taarifa ya kesi zilizopo mahakamani, majina ya watuhumiwa, tuhuma na hatua zilizochukuliwa kwa wakurugenzi waliodaiwa kufanya ubadhirifu sh milioni 444 katika mradi wa maboresho ya serikali za mitaa ikiwemo wizara hiyo itoe ripoti za miradi ipi imetekelezwa katika sekta ya kilimo, afya, maji na elimu.
Dk. Kigwangalah ambaye ni mbunge wa Nzega alisema kuwa kwa mwaka 2014, kuwajibishana ni lazima ili kuendana na mabadiliko chanya katika kuwaletea wananchi maendeleo.

No comments:

Post a Comment