Monday, 9 September 2013

KINANA, NAPE KUWASILI SHINYANGA KESHO SAA TATU ASUBUHI

Sep 9, 2013
Ndugu Kinana
SHINYANGA, Tanzania
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana kesho Jumanne, ataanza ziara ya siku nne mkoani Shinyanga kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM na uhai wa Chama.

  akiwa mkoani Shinyanga Kinana atakagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika wilaya zote za mkoa huo sambamba na kutoa kadi kwa wanachama wapya wa CCM ambapo pia atafanya vikao vya ndani ikiwa ni moja ya mikakati ya uimarishaji wa chama mkoani humo.

Katibu wa CCM mkoani Shinyanga, Adam Ngalawa amesema leo kwamba Kinana na msafara wake akiwemo Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, CCM, Nape Nnauye, wanatarajiwa kupokelewa kesho saa 3 asubuhi katika kata ya Isaka wilayani Kahama wakitokea Nzega mkoani Tabora.

Ngalawa alisema baada ya kupokelewa kwa Katibu Mkuu akiwa katika kata ya Isaka atasaini kitabu cha wageni na kisha atapokea taarifa ya utekelezaji wa kazi za CCM za wilaya ya Kahama na mkoa kwa ujumla pamoja na taarifa ya serikali ya mkoa.

Akiwa katika kata hiyo Kinana atagawa kadi za CCM kwa wanachama wapya na kisha atawasalimia wananchi kabla ya kuelekea katika kata ya Mwendakulima ambako atakagua miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa kituo cha afya cha Mwendakulima.

Katibu mkuu huyo akiwa mjini Kahama atafanya shughuli mbalimbali ikiwemo kuweka jiwe la msingi katika ofisi ya CCM kata ya Majengo, kufungua shina la wakereketwa la Mkombozi SACCOS Majengo pia atakuwa na kikao cha ndani na viongozi wa kata, matawi, mabalozi, wazee na madiwani wa CCM wilayani Kahama.

Kesho mchana Kinana atakuwa na mkutano wa hadhara katika eneo la uwanja wa CDT ambapo keshokutwa jumatano ataelekea wilaya ya Shinyanga ambako atakagua shughuli mbalimbali za maendeleo katika wilaya hiyo na kushiriki katika ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo pia atakuwa na mkutano wa hadhara katika kijiji cha Salawe.

Pia katibu huyo ataendelea na ziara yake katika wilaya za Kishapu na Shinyanga manispaa ambako pia atakuwa na shughuli za kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama ilivyoainishwa ndani ya ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010.

Kinana ataondoka mkoani Shinyanga Septemba 14, mwaka huu kwenda katika mkoa mpya wa Simiyu ambako pia atafanya shughuli za kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM na uimarishaji wa chama katika wilaya zote za mkoa huo.

No comments:

Post a Comment