Tumeona ya Futari, Tusisubiri ya Kwaresma!
Ukistaajabu ya Musa, utayaona ya
Firauni! Nilidhani kuwaona wanasiasa wanageuka waongoza Ibada ndiyo ingekuwa
mwisho wa kustaajabu kwangu maishani. La hasha kumbe ndo bado kabisa vituko ndo
viko arif!
Toka nizaliwe sijapa kuona tukio
la kiibada lililogeuka kuwa msimu wa maonyesho ya kidunia kama Ramadhani ya
mwaka huu. Sote tumemuona Rais wetu mkarimu wakiwafuturisha watu wake wa nguvu
hususani wasanii, tumeona mabenki, makampuni ya simu na makampuni mengine
yakifuturisha wateja wao, tumesikia Manispaa zikifuturisha, tumeona wabunge
wengi tu wakitoa vitu vya kufuturisha katika majimbo yao, tusimsahau Mama Salma
naye hakubaki nyuma. Wote hawa hawafuturu na walengwa ikabaki kuwa ibada yao ya
sirini bali huakikisha pia uwepo wa vyombo vya habari kama sehemu kuu ya ibada
yao. Na leo tunasoma habari za Edward Lowassa kufuturu Tanga. Nimevutiwa na
Mtiririko huu wa jinsi matukio ya Kiibada yalivyogeuka majukwaa ya kisiasa na
taratibu Wanasiasa wanavyozidi kujichukulia kiti kwenye mimbari na altare huku
Wachungaji, Mashehe na Mapadri wakigeuka kuwa waumini na walei wakati waumini
na walei wao wakichukua jukumu jipya ndani ya makanisa na msikiti kama
washangiliaji. Nani ataliokoa kanisa la Mungu na wanyanganyi? Mtume gani
atarudi kuzikomboa Masjid za mwenyezi Mungu?
Naamini katika matendo ya sadaka
za kiibada lakini siamini katika show-off za namna ya ufuturishaji
unavyofanywa. Naamini sadaka ya kweli ni ile mtu anayotoa moyoni si kwa ajili
ya kuufamisha umma anafanya nini bali kwa ajili ya kumfurahisha muumba wake.
Sote tumeona jinsi ufuturishaji ulivyogeuka kuwa sehemu ya CSR ya Makampuni na
majukwaa ya kisiasa. Mwanzo miaka ya nyuma tulizoea makampuni ya simu ndiyo
yalikuwa yanatumia ufuturishaji lakini sasa tumeona na wanasiasa wamevamia kwa
kasi ya ajabu mlango huu. Kama mwenendo huu unahusiana na harakati za mwaka
2015, basi natabiri mwakani kuna wanasiasa na vyama vya siasa vitafuturisha
mwezi mzima! Tutainajisi futari na itageuka chanzo cha kututenganisha. Wapo wataoanza
kusema “mie nafuturu msikiti wa chama Fulani” na wengine watakuwa wanashiriki
“futari ya mgombea fulani”
Tumebomoa misingi ya nchi, kila
uchao tunavunja miiko ya vyama, tunahimiza na kutekeleza itikadi za kibaguzi,
na baada ya kuharibu huko kote sasa tumevamia kuivunja misingi ya ibada za
Mwenyezi Mungu?! Tutafakari upya tujirudi mapema. Tuwaambie hapana wanasiasa
uchwara wanaotusababishia maisha magumu na njaa ili watuhadae kwa futari la
msimu. Tutumie hekima na busara kuwakosoa viongozi wetu wa dini kwa kukumbatia
ukengeufu wa namna hii kujongea patakatifu. Tusipofanya hivyo sasa, natarajia
msimu ujao itakuwa zamu ya matukio haya haya kudurufiwa katika Kwaresma. Na
ndipo katika madhehebu yote, tukio hili la ibada ya toba litakapokuwa limegeuka
rasmi kuwa mateka na jukwaa la wanasiasa. Tumeona ya Futari, Tusisubiri ya
Kwaresma kuchukua hatua!
Ni mtazamo wa Erick Kimasha,
msomaji na mchangiaji wa hii Blog.
No comments:
Post a Comment