Thursday, 15 August 2013

APEWA Tshs 120.000 KUTOROSHA TWIGA UWANJA WA KIA



Shahidi wa 10 katika kesi ya usafirishaji wanyama hai nje ya nchi amemtaja mshitakiwa wa kwanza, Kamran Mohamed, ambaye ni raia wa Pakistan kuwa alimzawadia Sh. 120,000 kwa ajili ya kazi aliyoifanya ya kupakia wanyama hao kwenye ndege ya Qatar Airforce Novemba 25, 2010.

Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Kobelo, shahidi huyo ambaye ni mfanyakazi wa Kampuni ya Swissport International inayohudumia mizigo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Ally Mzava, alidai mahakamani kuwa siku hiyo alipewa taarifa kuwa kutakuwa na ndege ya dharura.

Kwamba, ndege hiyo itafika KIA usiku na kupakia ndege, hivyo alitakiwa kuwataarifu wenzake ili wawe tayari kwa ajili ya kupakia wanyama hao.


Mzava alidai kuwa mara baada ya kupewa taarifa hiyo kutoka kwa mkuu wa kitengo cha ndege za dharura aliyemtaja kwa jina la Rosemary Michael, aliwaandaa wenzake na baada ya ndege hiyo kufika KIA, walianza kupakia mizigo hiyo, ambayo ilikuwa imefungwa kwenye maboksi.

“Tuliifanya kazi hiyo kwa umakini. Tukiwa ndani ya ile ndege pale pale uwanjani, nilipewa Sh. 120,000 kama ‘tip’ (bakshishi) ya kazi tuliyoifanya na kuambiwa na Mhindi aliyekuwamo mle ndani kuwa nigawane na wenzangu…ninamfahamu ni yule Mhindi pale nasikia wanamwita Kamran,” shahidi huyo aliiambia mahakama.

Alidai baada ya kumaliza kazi hiyo, aliondoka na hakujua kilichoendelea kutokana na kazi aliyotakiwa kuifanya kukamilika.

Shahidi huyo alidai ndege hiyo ilikuwa imeandikwa ubavuni jina la Qatar Airforce One.
Shahidi mwingine, Joseph Mpimbwe, ambaye ni msimamizi katika Kampuni ya Swissport iliyopewa dhamana ya kupakia na kushusha mizigo kwenye ndege KIA, alidai aliona twiga wawili wakipakiwa kwenye ndege.

Mbele ya Hakimu Kobelo, shahidi huyo alidai katika tarehe hiyo alipigiwa simu na Rosemary na kupewa taarifa ya kuwapo kwa ndege itakayosafirisha wanyama usiku wa manane. Alidai kuwa baada ya kupigiwa simu hiyo, alimpigia simu Moris Njau na kumpa taarifa hiyo ili awaandae wafanyakazi wenzake kwa ajili ya upakiaji wa wanyama hao.

“Nilipata bahati ya kuona twiga wawili wakiwa wamefungwa kwenye boksi na kulikuwa na vifurushi vingi vilivyokuwa vimefungwa. Siyo mara ya kwanza kupakiza wanyama,” aliiambia mahakama na kuongeza:

“Na tumekuwa tukifanya hivi mara kwa mara, ndege iliondoka kesho yake asubuhi baada ya sisi kumaliza kupakia wanyama hao. Ilikuwa saa 12:00 kasoro,” alidai.

Hata hivyo, shahidi huyo alidai hawawezi kupakia mzigo kwenye ndege bila ya kuwa na kibali kinachoeleza aina ya mzigo, uzito wake na anayehusika nao (cargo manifest), ambayo inaelezea aina ya mzigo unaopaswa kupakiwa au kushushwa kwenye ndege.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 24, mwaka huu mashahidi wengine watakapoendelea kutoa ushahidi wao.

Wanyama hao wanadaiwa kutoroshwa kwa kutumia ndege ya Quatar Emiri Air Force kwenda Doha, nchini Qatar, Falme za Kiarabu kupitia KIA. Inadaiwa kuwa wanyama aina tofauti 144 na ndege pori wawili.

Katika orodha hiyo, inadaiwa kuwa kulikuwa na twiga na viroba vya nyama pori ya kukausha zaidi ya tani tano.

Utoroshaji huo unadaiwa kuwa uliikosesha serikali zaidi ya Sh. milioni 170. Ilidaiwa kuwa wanyama hao walipakiwa usiku wa manane Novemba 24, 2010 na kuwa kampuni ya uwindaji wanyama ya Ham Marketing na Kampuni ya Uwindaji Ndege ya Luwego Bird Trappers ndizo zilizokamata wanyama hao na ndege
.

No comments:

Post a Comment