Wednesday 6 November 2013

Nani awajibike ujenzi ghorofa mbovu K’koo?


Meneja Uendeshaji wa Kampuni ya Design Plus Architects, Mustafa Maulid akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam  kuhusu ukaguzi wa majengo 67 yaliyojengwa kinyume na utaratibu na chini ya kiwango eneo la Kariakoo. Kushoto ni Mhasibu wa Kampuni hiyo, Zaina Nassor.

Kariakoo ni eneo kubwa lenye msongamano mkubwa wa watu, kwani ndio kituo chenye mkusanyiko wa watu kutoka wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam na sehemu nyingine, ikiwamo Zanzibar.


Jana tulichapisha habari ya kutia hofu na iliyoashiria kwamba upo uwezekano mkubwa wa wananchi wengi kupoteza maisha wakati wowote kutokana na Sekta ya Ujenzi kuendeshwa kiholela na bila usimamizi wa viwango. Kampuni ya Design Plus Archtects (DPA), ambayo ilipewa zabuni ya kufanya ukaguzi wa majengo katika Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam imegundua kuwa, kati ya majengo ya ghorofa 90 yaliyokaguliwa katika manispaa hiyo, 67 yamejengwa chini ya kiwango na kinyume na sheria.
Msemaji wa kampuni hiyo ya DPA, Mustafa Maulid aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi kwamba hali ni mbaya katika majengo waliyoyakagua, huku akisema majengo hayo yana nyufa nyingi na yanaweza kuporomoka wakati wowote. Uamuzi wa kuipa kampuni binafsi kazi ya kukagua majengo ulikuja baada ya jengo lenye orofa 16 katika manispaa hiyo kuanguka Machi 26, mwaka huu na kuua watu 36, mbali na majengo mengine yaliyoanguka na kusababisha maafa makubwa huko nyuma.
Tunasema hizi ni habari za kutia hofu kutokana na ukweli kwamba hali hiyo mbovu ya majengo siyo tatizo la Manispaa ya Ilala pekee, bali pia ndiyo hali ya majengo katika maeneo mengi ya miji yetu hivi sasa. Sekta ya Ujenzi katika nchi yetu katika miaka ya hivi karibuni inaweza kufananishwa na mtoto yatima aliyeachwa duniani pasipo usimamizi au matunzo stahiki ya kumfanya aishi maisha ya heshima na katika mazingira yasiyo ya udhalilishaji. Hofu pia inatokana na mamlaka zilizopewa dhima ya kusimamia Sekta ya Ujenzi kushindwa kufanya hivyo kutokana na kugubikwa na vitendo vya rushwa na ufisadi.
Kariakoo ni eneo kubwa lenye msongamano mkubwa wa watu, kwani ndio kituo chenye mkusanyiko wa watu kutoka wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam na sehemu nyingine, ikiwamo Zanzibar. Tunaambiwa hata kama siyo mtaalamu wa ujenzi, ukipita Kariakoo utagundua kwamba majengo mengi ya ghorofa yamejengwa bila kuzingatia sheria za ujenzi.
Hali hiyo imethibitishwa pia na Kampuni ya DPA iliyofanya ukaguzi wa majengo katika Manispaa ya Ilala. Kampuni hiyo inasema imegundua watu wengi wanafanya ujenzi bila vibali, wanajenga bila kufuata michoro iliyoidhinishwa na Manispaa ya Ilala na watu wanahamia kwenye majengo ya ghorofa kabla ujenzi wake haujakamilika. DPA pia inasema majengo yanatofautiana na michoro iliyotoka kwa wataalamu husika. Kwa mfano, pamoja na majengo yote ya Kariakoo kutakiwa kuwa na maegesho ya magari, wajenzi wameweka fremu za maduka.
Bahati mbaya hata Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa hana jibu sahihi kuhusu nini kifanyike. Kwa kudhani kwamba vikao vya madiwani ndivyo vitakavyotoa jibu kuhusu tatizo hilo, Meya Silaa anaonyesha bayana kwamba hata yeye hajui ukubwa wa tatizo hilo. Pamoja na kwamba kisheria madiwani ndio wenye dhima ya kusimamia sera za ukuaji wa miji, matatizo yaliyobainishwa na DPA ni mazito mno kutatuliwa na madiwani hao.
Sisi tunadhani mamlaka ya kufanya uamuzi mgumu kuhusu ghorofa nyingi mbovu za Kariakoo na kwingineko ni Serikali Kuu, ambayo pamoja na mambo mengine inapaswa kuwawajibisha walioshindwa kuzuia ujenzi holela. Hapa tuna maana kwamba uamuzi huo ufanywe na Waziri Mkuu, Makamu wa Rais au Rais mwenyewe.

No comments:

Post a Comment