Tuesday, 5 November 2013

MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA UONGOZI WA SELCOM WIRELESS TANZANIA IKULU, DAR ES SALAAM

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na baadhi ya Viongozi wa Selcom Wireless Tanzania, Meneja Miradi wa Selcom, Gallus Runyeta (katikati) akitoa maelezo kuhusu shughuli zinazofanywa na Selcom. (kushoto) ni Meneja Masoko na Muendesha Biashara, Juma Mgori.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na baadhi ya Viongozi wa Selcom Wireless Tanzania, Meneja Miradi wa Selcom, Gallus Runyeta (katikati) akitoa maelezo kuhusu shughuli zinazofanywa na Selcom. (wa pili kushoto) ni Meneja Masoko na Muendesha Biashara, Juma Mgori na Mhandisi wa Software, Godfrey Kiapinga.
********************************

Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amekutana na Uongozi wa Kampuni ya Selcomwireless Tanzania na kufanya nao mazungumzo ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam Jumatatu Novemba 04, 2013. Uongozi wa Selcomwireless uliofika kukutana na Mheshimiwa Makamu ulikuwa pamoja na Meneja Miradi wa Selcom (Gallus Runyeta), Meneja Masoko na Muendesha Biashara (Juma Mgori) na Mhandisi wa Software (Godfrey Kapinga).

Wakiwa katika mazungumzo na Mheshimiwa Makamu wa Rais, Meneja Miradi wa Selcomwireless Tanzania Gallus Runyetta alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa, kampuni yao ambayo imejikita katika kutoa huduma za malipo ya Kielekroniki imekuwa ikifanya miradi mbalimbali ambayo imerahisisha malipo kwa wananchi wa Tanzania ikiwa ni pamoja na malipo ya umeme wa Luku na sasa iko katika hatua za mwisho za kuzindua ushirikiano na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu uthaminishaji wa malipo ya magari hali ambayo itasaidia kupunguza usumbufu kwa wanaoagiza magari nje ya nchi.

Uongozi wa Selcomwireless pia ulimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa, Selcom inazidi kujitanua katika kutoa huduma za malipo sambamba na takwimu katika maeneo ya afya na mfano mzuri ni Zanzibar ambako huko Selcomwireless imeshiriki katika harakati za kutokomeza Malaria, harakati ambazo pia inashiriki kwa upande wa Tanzania Bara.

Mheshimiwa Makamu wa Rais aliwataka Selcomwireless kuendelea kuisaidia nchi hasa katika suala zima la kukusanya mapato na akawataka kuhakikisha wanakutana na Uongozi wa Mfuko wa Bima ya Afya ili kuwapa namna ya kusaidia wananchi hasa wa vijijini kulipia Bima zao kwa gharama wanazoweza kumudu.

“Mkiwasaidia watu wa Bima ya Afya na kuwafanya walipaji kuwa wanalipa kidogo kidogo kwa vipindi fulani inaweza kabisa kubadili hali ya huduma za afya hapa nchini,” alisema na kuongeza: “Tunakutegemeeni sana na jitahidini kutumia nafasi hizi ili kuhakikisha kuwa wananchi wengi wanajitokeza kulipia Bima za afya kwa kuwarahisishia namna ya kupata huduma”.

Mheshimiwa Makamu wa Rais pia aliwataka Selcomwireless kutafuta namna ya kutatua changamoto ya ulipaji wa kodi za nyumba sambamba na kukutana na viongozi wa Wizara ya Ardhi, ili watu walio na Hati zao za viwanja na makazi waweze kulipa kodi zao kwa mtandao ili kurahisisha ukusanyaji na pia kutanua wigo wa mapato katika manispaa hapa nchini.

No comments:

Post a Comment