Askari wa FFU wakilinda doria katika kiwanda cha ufatuaji tofali cha Ujenzi Solutions, Kimara Dar es Salaam |
Moja ya mabomba linalodaiwa kuunganishwa kiholela kwenye bomba kuu la Ruvu Juu linaloleta maji mjini na kampuni ya Ujenzi Solutions eneo la Kimara |
Makalla akizungumza mbele ya Lori la Maji lililokamatwa likijazwa maji yanayodaiwa kuwa ya Dawass, katika kiwanda cha matofali cha Ujenzi Solutions |
Pumpu iliyonaswa na Dawasa ikinyonyonya maji kutoka bomba kuu la Ruvu Juu eneo la Ubungo, Dar es Salaam |
Makalla akiondoka katika kiwanda cha matofali cha Moto ambacho alisitisha shguli zake baada ya kubainika wakiiba maji ya Dawasa eneo la Ubungo. |
Ramani ya upanuzi wa Mtambo wa Maji wa Ruvu Juu, eneo la Mlandizi, Pwanik. |
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa akijaribu kuendesha katapila la Kampuni ya Wagani ambayo imepewa tenda ya upanuzi wa Mtambo wa Maji wa Ruvu Juu. |
Makalla
(wa pili kushoto) Mbunge wa Kihaha Vijijini, Hamoud Jumaa ( wa pili
kulia) na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Halima Kihemba kulia, wakikagua
ujenzi wa upanuzi wa mtambo huo. Picha na Richard Mwaikenda
Na Richard Mwaikenda
NAIBU Waziri wa Maji, Amos Makalla amezifungia kampuni tatu za
ufyatuaji tofali kuendesha shughuli baada ya kubainika kujiunganishia
isivyo halali maji kutoka kwenye bomba kuu la Mamlaka ya Maji Safi na
Taka (DAWASA), wakati wa ukaguzi wa kushitukiza alioufanya leo katika
Mkoa wa Dar es Salaam.
Makalla aliamuru viongozi wa kampuni hizo wakamatwe na kufikishwa
kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi, ambapo pia aliagiza mali zote
za kampuni hizo zifilisiwe ili zitumike kulipa fidia kwa hasara kubwa
iliyoingizia Serikali.
Akiwa katika ukaguzi huo, Makala aligundua madudu mengi yanayofanywa
na kampuni hizo, ambazo zimejiunganishia maji kwa ajili ya kufyatulia
matofali na kuuza kwa kutumia malori.
Kampuni alizozikagua leo na kukutwa na dhahama hiyo ni; Moto iliyopo
mita chache kutoka Makao Makuu ya Wizara ya Maji, Ubungo Dar es Salaam,
Ujenzi Solutions iliyopo Kimara kwa Msuguri pamoja na kampuni isiyo na
jina iliyopo pia Kimara kwa Msuguri.
Kabla ya kufika katika kampuni hizo, ulinzi wa Polisi wenye silaha
ulikuwa umeimarishwa, ambapo Makalla alitoa agizo kwamba wasiondoke
katika maeneo hayo ili wahusika na wafanyakazi wao wasiendelee na kazi
yoyote.
Katika kampuni ya Moto, ilikutwa pampu ikiendelea na kazi ya kuvuta
maji ambapo Msimamizi wa kampuni hiyo, Frederick Tarimo alikana kuiba
maji kwenye bomba la Dawasa na kudai kwamba maji hayo wanayatoa kutoka
kwenye mto.
Tarimo alisema kuwa hutumia lita 3000 za maji kwa siku, ambapo
hufyatua matofali kati ya 1500 na 2000 kwa siku. Pia huuza kwa siku
kiasi cha matofali kama hayo. Kila tofari huuzwa kati ya sh. 800 na
1000. Alisema kuwa endapo hatofanya kazi kwa muda wa mwezi mmoja
ataingia hasara ya sh. mil. 90, hivyo kila siku kupata hasara ya sh.
mil. 3.
Naye Meneja wa kampuni ya Ujenzi Solutions, Rahim Hamis, alikana
katakata kwamba maji wanayoyatumia wameunganisha kutoka kwenye bomba la
Dawasa, bali wanatumia maji kutoka kwenye bwawa dogo lililopo jirani na
kampuni yao. Pia katika eneo hilo lilikamatwa lori aina ya Isuzu namba
957 AJK likijazwa maji.
Viongozi waliokamatwa ni Frederck Tarimo ambaye alijitaja kuwa
msimamizi wa kampuni ya Moto, Meneja Mkuu wa kampuni ya Ujenzi
Solutions, Rahim Hamis na Credo Rajab mmiliki wa kampuni aliyodai haina
jina.
Makalla, alisema ili kupambana na wezi wa maji, haina budi sasa
kupeleka mswada bungeni ili watungiwe sheria ya uhujumu uchumi pamoja na
kutoa adhabu kali ikiwemo ya kutaifisha mali zao, tofauti na adhabu
wanayopewa sasa ya kulipishwa faini ya sh, mil 2.
Katika ziara hiyo pia alifanya ukaguzi wa matanki ya kuhifadhia maji
ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo alijionea jinsi maji
yalivyopungua kwenye matanki hayo ambayo pia yapo kwenye maandalizi ya
kufanyiwa ukarabati mkubwa ili yafae kwa ajili ya hifadhi ya maji kutoka
bomba la Ruvu Chini ambalo upanuzi wake umekamilika.
Pia alitembelea kuona maendeleo ya upanuzi wa Mtambo wa Maji wa Ruvu
Juu, Chalinze, Mkoa wa Pwani. kesho anaendelea tena na ziara kama hiyo
katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.
No comments:
Post a Comment