CCM KUZIPITIA MWEZI UJAO ADHABU ILIZOWAPA WAWANIA URAIS, YARIDHISHWA NA MAZUNGUMZO YA VYAMA CHINI YA MSAJILI WA VYAMA
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema, mwezi ujao, kitafanya mapitio ya utekelezaji wa adhabu walizopewa baadhi ya wanachama kwa kukia taratibu za kuwania Urais, ikiwemo kujitangaza mapema.
Kimesema, Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama itafanya mapitio ya mwenendo wa utekelezaji wa adhabu walizopewa na Kamati Kuu mapema mwaka huu, na kama itabainika kuwa hawatekelezi ipasavyo masharti ya adhabu zao, itapendekeza kwa Kamati Kuu kuongezwa kwa adhabu kulingana na ukubwa wa uvunjaji wa masharti ya adhabu husika.
Hayo yamesemwa leo, na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, akieleza maamuzi yaliyofikiwa katika Kikao cha Kamati Kuu ya CCM, kilichofanyika jana, mjini Dar es Salaam, chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
"Kamati Kuu ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM walioonesha nia ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea Urais. Baada ya kutafakari kwa kina, Kamati Kuu inapenda kuwakumbusha wote kuwa ili wasipoteze sifa za kugombea, ni muhimu wakazingatia Katiba, Kanuni na taratibu za Chama zinazosimamia masuala hayo", amesema Nape na kuongeza.
Nape alisema, ni muhimu wanachama wote wakakumbuka kuwa Chama ni pamoja na Katiba, Kanuni na taratibu zake, hivyo kutoziheshimu na kuzifuata ni kukivuruga, jambo ambalo halivumiliki.
Alisema, nia ya CCM kusimamia hayo ni kuhakikisha Chama kinakuwa na umoja na mshikamano ambao ni muhimu sana, hasa Chama kinapoelekea kukamilisha kazi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010/2015 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Nape alisema, pia kikao hicho cha Kamati Kuu, kilipokea taarifa ya mazungumzo yanayoendelea kati ya CCM kwa upande mmoja na CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kwa upande wa pili.
Alisema, mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi yana lengo la kuangalia kwa kina ni kwa nini baadhi ya wajumbe wachache wa Bunge Maalum la Katiba walisusia na kutoka nje katika awamu ya kwanza ya Bunge hilo, na kuangalia namna watakavyorudi ili kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba nchini.
Nape alisema, kwa ujumla Kamati Kuu ya CCM imeridhishwa na mwenendo wa mazungumzo hayo na kupongeza juhudi hizo zilizofanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa na Vyama husika.
"Kamati Kuu inapenda kueleza imani yake kuwa mazungumzo hayo yatazaa matunda kwa wajumbe wachache waliosusia Bunge Maalum la Katiba, kurejea Bungeni na kumalizia sehemu ya mchakato uliobakia. Kamati Kuu inayatakia kila la kheri mazungumzo hayo", alisema Nape.
Aidha, Kamati Kuu imewatakia kheri na fanaka Watanzania wote wakati huu wanapomalizia mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
No comments:
Post a Comment