SSP ADVERA SENSO
Tunapoelekea kipindi hiki cha sikukuu ya Pasaka, Jeshi la Polisi nchini,
linatoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini katika suala la usalama wa
maisha na mali zao.
Uzoefu unaonyesha kwamba, katika kipindi kama hiki cha sikukuu kuna
baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo kufanya vitendo vya uhalifu.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi katika mikoa yote limejipanga vizuri kwa
kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba
hakuna vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza na endapo
vitajitokeza viweze kudhibitiwa kwa haraka.
Aidha, ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote, yakiwemo maeneo ya
kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine ambayo
yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.
Vilevile, Jeshi la Polisi linawataka madereva na watu wote watakaokuwa
wakitumia barabara, kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama
barabarani, kuepuka kwenda mwendo kasi, kujaza abiria kupita kiasi na
kutumia vilevi wawapo kazini.
Wamiliki wa kumbi za starehe wazingatie uhalali na matumizi ya kumbi zao
katika uingizaji wa watu kulingana na uwezo wa kumbi hizo, badala ya
kuendekeza tamaa ya fedha kwa kujaza watu kupita kiasi.
Aidha, wazazi wawe makini na watoto wao, kutokuwaacha watembee peke yao
ama kwenda disko toto bila kuwa chini ya uangalizi wa watu wazima ili
kuepusha ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu
yao.
Wananchi wakumbuke kutokuacha makazi yao bila uangalizi na endapo
italazimu kufanya hivyo watoe taarifa kwa majirani zao, na pale
wanapowatilia mashaka watu wasiowafahamu wasikae kimya, watoe taarifa
haraka kwenye vituo vya polisi vilivyo karibu yao, ili hatua stahiki
ziweze kuchukuliwa haraka.
Mwisho, Jeshi la Polisi linapenda kuwashukuru wale wote ambao tayari
wamefunga kamera za CCTV katika maeneo yao ya biashara hususani yale
yanayokuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu, yakiwemo maduka, mahoteli na
maeneo ya benki.
Jeshi la Polisi linaendelea kuwasisitiza ambao bado hawajaweka kamera
hizo, kuweka ili ziweze kusaidia kubaini wahalifu na hata kurahisisha
ukamataji wa wahalifu hao endapo uhalifu unatokea.
Tunawatakia Watanzania wote Pasaka njema.
No comments:
Post a Comment