Sunday, 20 October 2013

UTATA MPYA UJIO WA ALEX MASSAWE





HATUA za kumrejesha nchini mfanyabiashara maarufu, Alex Massawe, aliyefikishwa mahakamani nchini Dubai, Falme za Kiarabu (UAE) kwa tuhuma za mauaji, zimegubikwa na utata mkubwa, huku Tanzania ikidaiwa kushindwa kutimiza masharti ya Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol).

Kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka Dubai, Interpol iliipa Tanzania hadi kufikia Septemba 4, mwaka huu, iwe imewasilisha vielelezo vya kuthibitisha tuhuma zake.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa muda huo umemalizika bila Tanzania kuwasilisha uthibitisho huo na kwamba Massawe ameachiwa huru nchini humo.

Massawe alikamatwa Dubai kati ya Juni 20 na 25. Kwa mujibu wa Mkuu wa Interpol, Tawi la Tanzania, Gustav Babile, ombi la kumleta mhalifu nchini kutoka nje ya nchi (extradition request) lina hatua ndefu.

Alisema kuwa kuna mlolongo wa taratibu za kutekeleza ili Massawe aletwe, akasisitiza kuwa ilikuwa ni lazima kwanza Polisi wa Tanzania watoe tangazo kwa Interpol kuhusu kumsaka mtu huyo ili aletwe.

Jeshi la Polisi nchini limekanusha taarifa hizo za kuachiwa kwa Massawe, likisema halina taarifa za suala hilo, na kwamba taratibu za kisheria zinaendelea kufanyika.

Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso, alisema: “Mambo ya kusikia sisi hatuyafanyii kazi, kwanza vyanzo vingine vya habari ni vya kutiliwa shaka. Sisi tukijiridhisha tukawa na taarifa kamili tutawaambia.”

No comments:

Post a Comment