SIRI imefichuka. Mbio
za Edward Lowassa, kusaka urais kwa udi na uvumba, zimebarikiwa kwa asilimia
100 na Rais Jakaya Kikwete.
Lowassa amekutana na Kikwete mara kadhaa
na kufunga makubaliano ya siri yanayolenga kumsaidia yeye kuwa mgombea urais
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Pendo Omary …
(endelea).
“ Yote yanayofanywa na Edward (Lowassa),
yamebarikiwa na Kikwete. Bila hivyo, Lowassa asingekuwa na ubavu wa kufanya
anachokitenda,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya serikali.
Kikwete ndiye
Mwenyekiti wa Taifa wa CCM na Rais wa Jamhuri.
Kuibuka
kwa taarifa kuwa Lowassa amefunga makubaliano na Kikwete, kumekuja katika
kipindi ambacho mwanasiasa huyo aliyeapa kufia katika vita ya kuwania madaraka,
ameanza kupokea makundi ya wananchi akidai wanamuomba kugombea urais.
Mtoa taarifa wa Mtandao huu anasema,
“Kikwete na Lowassa wanakutana sana, tena kwa siri. Wamejadili mengi, ikiwamo
kinyang’anyiro cha urais. Itakuwa ajabu, bwana huyu kutokuwa mgombea kupitia
CCM.”
Waziri mkuu huyo aliyejiuzulu
kwa kashfa ya mkataba tata wa kufua umeme, kati ya serikali na kampuni ya
Richmond, tayari amefungulia anaowaita “wafuasi wake,” kushawishi baadhi ya
watu kwa lengo la kutafuta kila upenyo kuhakikisha anapata nafasi ya kushika
utawala Oktoba mwaka huu.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka kwa watu walio karibu na mwanasiasa huyo, makubaliano
yake na Kikwete ndiyo yanayomfanya kuwa “mbogo” hadi kuikuka taratibu za chama
chake.
Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika
mwishoni mwa Oktoba mwaka huu – kuchagua rais, wabunge na madiwani.
Hata hivyo, mtoa taarifa wa Chanzo chetu
anasema, pamoja na kuwapo makubaliano hayo, bado Lowassa hawezi kujihakikishia
nafasi ya kuwa mgombea.
Anasema, Lowassa anakabiliwa na kibarua
kigumu kutoka kwa makundi ya yaliyopachikwa jina la “wahafidhina” ndani ya
chama chake.
Kundi hilo ambalo limeapa kuhakikisha
Lowassa hawezi kupitishwa kuwa mgombea wa CCM, linaongozwa na Benard Membe,
waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa.
“Bado anakabiliwa na kazi ngumu mbele
yake. Ajenda ya kumzuia kuwa mgombea, inasukwa kwa ustadi mkubwa na watu kutoka
Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), ambao wengi wao wanamuunga mkono Membe,”
anaeleza.
Anasema, “…baadhi ya mahafidhina, baada
ya kushawishiwa na idara ya usalama, walitaka waongeze adhabu dhidi ya Lowassa
na wenzake ili ifikie hadi Februari mwakani. Hii itamfanya yeye na wenzake
kutogombea urais.”
Staili ambayo Lowassa ameamua kuitumia,
ndiyo ambayo ilitumiwa na Kikwete kuingia Ikulu mwaka 2005. Wakati huo Kikwete
na genge lake, waliunda kilichoitwa, “mtandao wa Kikwete mwaka 2005.”
Mtandao wa Kikwete ulitumia vyombo vya
habari; kukusanya watu na kuwalipa.
Mbio za Lowassa sasa zimefikia
mahali ambako, rais na mwenyekiti wa chama anakotoka, analazimika kutumia, siyo
tu busara, bali hekima na uamuzi wa “utu uzima.”
Lowassa na viongozi wengine watano
ndani ya CCM, “walitiwa hatiani” 18 Februari mwaka jana, kwa makosa ya
kujihusisha na kampeni za uchaguzi kabla ya wakati; kujenga mtandao wa kutafuta
urais kinyume cha maelekezo ya chama na kuanza kupenyeza fedha.
Wengine waliotiwa
“hatiani” ni pamoja na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe; Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Stephen Wasira; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
January Makamba na aliyewahi kuwa waziri wa nishati na madini, William Ngeleja.
Mpaka sasa bado wako kwenye kifungo
baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kuanza kampeni kabla ya wakati.
No comments:
Post a Comment