HAPO JUU NI BW SIMON MAKANGULA AMBAYE AFUNGWA HUKO MAREKANI
Mwenyekiti wa CCM wa tawi la Texas, Houston nchini Marekani, Simon
Makangula amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na nusu jela na kulipa
faini ya zaidi ya Sh92.4 milioni kwa kosa la kughushi nyaraka za ulipaji
wa kodi.
Makangula ambaye ni mmiliki wa kampuni ya kutoa huduma za malipo ya kodi
iitwayo Mshale Investment & Tax Service, alihukumiwa Ijumaa katika
Mahakama ya Wilaya na Jaji Gray Miller kwa udanganyifu huo wa kuwasaidia
wateja wake kughushi nyaraka za kodi ya mapato, kwa mujibu wa tovuti ya
click2houston.com.
Wakili wa serikali nchini humo, Kenneth Magidson pamoja na Lucy Cruz,
wakala maalumu wa kitengo cha uchunguzi wa makosa ya kihalifu katika
masuala ya mapato ya Marekani, kwa nyakati tofauti waliiambia mahakama
kuwa Makangula alimsaidia mmoja wa wateja wake ambaye ni raia wa
Marekani kutayarisha malipo ya kodi yasiyo halali.
Sambamba na kifungo cha mwaka mmoja na nusu, pia Makangula anatakiwa kulipa faini ya Dola 51,645 sawa na Sh92.4 milioni.
Oktoba 15, mwaka jana, Makangula alikiri kosa hilo mbele ya hakimu
Miller na kuwa malipo ya kodi hiyo yalikuwa na udanganyifu katika
vipengele kadhaa, yakiwamo katika makadirio na idadi ya wategemezi wa
mlipakodi, mambo yaliyosababisha hasara ya Dola 9,731 za Marekani
(Sh17.3 milioni).
Pia, katika kesi hiyo, Makangula alikiri kuwa alimsaidia mteja wake
kughushi kuwa yeye ndiye mmiliki pekee wa biashara hiyo, hatua
iliyosaidia watu wengine, washirika wa mteja wake, wakwepe kulipa kodi.
Kampuni ya Makangula inajishughulisha na huduma za ulipaji wa kodi,
uhasibu, mfumo wa ulipaji wa kodi za mapato, biashara za ardhi, kodi za
majengo na ushauri wa masuala ya kodi ya mapato.
Makangula, ambaye ni mwenyekiti wa tawi la CCM la Texas, anawaongoza
wajumbe tisa wa halmashauri ya tawi wanaoishi Marekani na mara kadhaa
ameonekana kwenye picha akiwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na CCM
wanaotembelea Marekani.
No comments:
Post a Comment