Dar
es Salaam. Hofu kuhusu nafasi ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu ujao inazidi
kuongezeka baada ya mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki
kukitabiria chama hicho tawala “kazi kubwa”, akisema hali ya sasa “siyo
ile iliyokuwa nayo miaka mitano iliyopita”.
Kagasheki
pia alikitahadharisha chama hicho dhidi ya kuzidi kukua kwa nguvu ya
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akisema iwapo umoja huo utamchagua
mgombea makini, CCM itakuwa na kazi ngumu.
Balozi
Kagasheki, ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii kabla ya
kujiuzulu kutokana na sakata la Operesheni Tokomeza, alisema hayo
mwishoni mwa wiki wakati wa mahojiano maalum na gazeti la Mwananchi.
Kauli
yake inaungana na za vigogo wengine wa CCM waliotahadharisha mwenendo
wa chama hicho dhidi ya ongezeko la nguvu ya upinzani, akiwamo Waziri
Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, ambaye alisema rushwa inakimaliza chama
hicho, na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba,
ambaye alisema kuwa chama hicho kisitegemee ushindi wa kishindo.
Akijibu
swali la maoni yake kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao na nafasi ya CCM,
Kagasheki alisema: “Ipo kazi, nafasi ya CCM sasa... Jamii imeanza kuwa
na maswali mengi kuhusu chama chetu, viongozi wachukue hili kwa umakini,
wakifuatilia watajua.”
Mbunge
huyo alisema kuwa matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa hivi
karibuni yametokana na wananchi kuona CCM imeshindwa kuisimamia vizuri
Serikali.
Katika
uchaguzi huo uliofanyika Desemba mwaka jana CCM ilishinda kwa asilimia
79.81 (vijiji) na 79.83 katika vitongoji, wakati kwenye mitaa mingi
ikiwa maeneo ya mijini kimeshuka kikipata asilimia 66.66, ikilinganishwa
na ushindi wa asilimia 89.2 katika mitaa, asilimia 91 katika vitongoji
na asilimia 91.6 katika vijiji katika uchaguzi huo mwaka 1999.
Kwa
mujibu wa matokeo hayo, kulikuwa na ongezeko kubwa la ushindi wa
wapinzani kwenye baadhi ya maeneo, hasa kutokana na kusimamisha mgombea
mmoja chini ya Ukawa inayounganisha vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi
na NLD.
“Mengine
yametokana na CCM kutoisimamia vizuri Serikali au kutotimiza wajibu.
Wapo wananchi wanaosema CCM inakumbatia waovu. Kama inataka kuendelea
kuaminika na kutumainiwa, CCM isibweteke, isione aibu kuikosoa Serikali.
“Hapa
natambua juhudi za Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana kuwa karibu na watu.
Ipo haja kwa CCM kujitazama upya, itazame mikakati yake, inaweza
kujipanga kurudisha imani.” Kauli hiyo ya Balozi Kagasheki imekuja siku
chache baada ya Makamba, ambaye ni mbunge wa Bumbuli kuwataka wanachama
wa chama hicho kikongwe kujiandaa kisaikolojia kwa matokeo yoyote
yanayoweza kutokea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
“Wana-CCM
wanatakiwa kujiandaa kisaikolojia kwani walizoea ushindi wa asilimia 90
au 80, huu ulikuwa ushindi wa nyuma. Tusishangae tukipata ushindi wa
asilimia 50, 60, 57 au 70 ni kitu cha kawaida kutokana na kukua kwa
demokrasia, hususan ushindani wa vyama vingi vya siasa kuanza
kuimarika,” Makamba alisema katika kipindi cha Power Breakfast cha Radio
ya Clouds.
No comments:
Post a Comment