Monday 20 January 2014

TUMEJIFUNZA NINI BUKOBA?

Maswali Magumu
KWA miezi minane mfululizo, gazeti la Tanzania Daima limekuwa linaandika habari za mgogoro wa Manispaa ya Bukoba, mkaoni Kagera, likifichua ufisadi wa Meya na wenzake, na kuunga mkono jitihada za  madiwani waliotaka Amani ajiuzulu.
Mgogoro haujaisha. Lakini hadi hapa tumepata mafunzo kadhaa. Kwanini nasema haujaisha?
Kwanza, nafasi ya meya iko wazi sasa. Kwa hiyo, harakati za kumpata meya mpya ndio zinaanza. Na kwa kuwa Amani ameondoka kwa kulazimishwa, na kwa kuzingatia hulka aliyoonyesha kwa muda wote huo, sina shaka ana kinyongo.
Kwa sababu hiyo, atajaribu kushiriki harakati za kuweka meya mwingine. Atakuwa kwenye kundi linalopinga wale walioshinikiza yeye aondolewe. Atataka kulipa kisasi kwa kusaidia,na  kuwezesha ushindi wa mshindani “asiye upande wake.”
Kimsingi, kwa kuwa naye ni diwani, ana haki zote kushiriki katika harakati za kupata meya mpya. Lakini katika mazingira yaliyomwondoa yeye, ushiriki wake huu unaweza kuwa chanzo cha mgogoro mpya iwapo viongozi wapya hawatakuwa waangalifu.
Pili, mgogoro huu haujaisha kwa sababu Amani amejiuzulu tu. Ndani ya kikao cha Baraza la Madiwani ambako alisomewa tuhuma zinazomkabili kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Ludovick Utoh, Amani alitiwa hatiani.
Kwa sababu hiyo, serikali, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, ililazimika kumtaka aondoke kwenye wadhifa wake. Ajabu ni kwamba kabla ya kujiuzulu, alipopewa fursa ya kusema, akakariri maneno ya Zaburi 23 “Bwana ndiye Mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu.”
Kwa juu juu tungeweza kusema hili ni neno la Mungu, na kwamba Amani alitamka maneno haya kama njia ya kuonyesha uumini wake na uchaji wake kwa Mungu. Lakini katika muktadha wa kilichomtokea, hii ni kauli ya jeuri.
Anadiriki kutumia Biblia kujikweza na kubeza wengine. Ni kauli ya majivuno. Alipaswa kuomba radhi kwa ufisadi aliokuwa amefanya na kuutetea kwa muda wote huo. Alipewa fursa ya kuonyesha uungwana, hakuitumia.
Huyo ndiye Amani. Bila shaka hilo nalo ni funzo muhimu tulilopata katika mgogoro huu. Uongozi uliojaa jeuri na dharau. Maana kama si jeuri, meya na watu wake wasingediriki kupitisha miradi ya mamilioni ya fedha bila vikao, au bila idhini ya madiwani ambao ni wawakilishi wa wananchi.
Funzo jingine ni kwamba imani ya dini imetumika vibaya. Watu wamefanya ufisadi wa wazi katika kutafuna raslimali za umma, halafu wakadiriki kujificha kwenye koti la dini.
Ghafla, zikaanza kusambazwa propaganda kwamba wanaompinga Amani ni kundi la Waislamu wasiopenda kuona Mkristo anaongoza Manispaa. Ujinga mtupu!
Tena baadhi yao wakadiriki kutumia hata viongozi wa kidini kumtetea Meya. Na ili watimize azima yao hii, wakataka kutuondoa kwenye hoja, wakidai kwamba mgogoro huu unatokana na ugomvi binafsi kati ya Mbunge wa Bukoba Mjini Khamis Kagasheki na Amani.
Wakadai Kagasheki amegundua kuwa Amani nataka ubunge, na kwamba miradi inayosimamiwa na Amani ikijengwa hataweza kumpiku kwenye kinyang’anyiro cha kugombea ubunge 2015.
Wasio na taarifa na wasiopenda kutafiti wakalibeba hilo kana kwamba ni kweli, bila kujua kuwa Manispaa ya Bukoba ipo ndani ya Jimbo la Bukoba Mjini.
Maana yake ni kwamba iwapo miradi hiyo ingefanikiwa, mbunge angeweza kuitumia kujinadi kwa wananchi kwa kuwa iko katika eneo lake. Angedai kwamba ametekeleza ilani ya chama chake – kama walivyozoea kusema.
Hilo nalo ni funzo, kwamba wananchi wetu wengi hawajui hata kazi za madiwani na wabunge wao. Wapo waliomuona Amani kama mkombozi, hata kama angekwapua pesa popote na kujenga soko, kupima viwanja, kujenga sehemu ya kuoshea magari kifisadi.
Wapo waliomuona Amani kama Mkristo tu anayeonewa na Waislamu, bila kujali kwamba Ukristo ungemsaidia kuelewa haraka ujumbe wa madiwani wanaompinga, kujirudi na kuondoka madarakani kabla hajaumbuka.
Kama Amani angeondoka mapema, si ajabu hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali asingekwenda Bukoba kumchunguza kwa kasi hii. Kwa jinsi tulivyozoea, hata hili lingefunikwa kijanja janja, na Amani angeendelea kudunda.
Lakini sasa hilo haliwezekani tena. Haitawezekana kwa Amani kuendelea kudunda mitaani akiwa na tuhuma nyingi zilizothibitishwa na wakaguzi. Tunajua serikali mkoani Kagera na Wilaya ya Bukoba imekuwa inamkingia kifua, lakini siamini kwamba itaendelea kufanya hayo sasa.
Sitaki kuamini kwamba Jeshi la Polisi litashindwa kuchukua hatua za kumfikisha Amani katika vyombo vya sheria, kwani uchunguzi huu umefanywa na serikali, na ni uchunguzi makini; na ni kielelezo ambacho polisi wanapaswa kukitumia katika kumtendea haki Amani.
Na hapa kuna fundisho jingine. Kwamba baada ya Amani kuthibitishwa kuwa ameshiriki kufanya na kutetea ufisadi mkubwa katika Manispaa ya Bukoba, huku serikali ikimtaka aachie ngazi, jeshi la polisi lilishindwa kufanya kazi yake na kuondoka naye pale pale na kumpeleka alikostahili kwenda huku akisubiri kufikishwa mahakamani.
Walimuacha akaondoka kikaoni kama shujaa, akaenda kwake kana kwamba hakuna jambo lililotokea. Kumbe polisi wanaweza kutia watu kadhaa mbaroni, na kuwaacha wengine tena wenye makosa makubwa zaidi?
Wakati Amani anatembeea kifua mbele mitaani licha ya serikali kuthibitisha ufisadi wake, polisi wanahangaika kukamata madereva wa pikipiki na daladala wanaoegesha vibaya au wanaovunja sheria ndogo ndogo za barabarani.
Au wanahangaika kukamata na kusweka ndani vibaka wanaopora mikufu na heleni za kina mama barabarani. Mambo kama haya ndiyo yanawafanya wananchi wakose imani na jeshi la polisi na serikali.
Haya ndiyo yanafanya wananchi wanaasi na kugomea mambo ya msingi yanayopendekezwa na watawala. Wanaona wanaishi katika jamii isiyo na haki. Na kwa hakika, upendeleo huu wa serikali ndio unahatarisha amani ya nchi.
Katika mgogoro huu, tumejifunza pia kwamba serikali kutoka wilaya hadi taifa haikuwa na nia ya kutatua mgogoro huu.
Gazeti hili linajua, na wananchi wanajua pia, kwamba hata Rais Jakaya Kikwete alipotembelea Mkoa wa Kagera, baada ya kupewa taarifa za mgogoro huo, alitaka kuonyesha utani. Katika mkutano wa kuhitimisha ziara yake katika Uwanja wa Kaitaba, Rais Kikwete alijitumbukiza katika propaganda za “ugomvi  wa Amani na Kagasheki.”
Alifika mahali akasema “ugomvi huu wa watu wawili” unachelewesha maendeleo ya Bukoba. Akawataka “wawili” wapatane ili kazi ziendelee.
Wanafiki wakapiga makofi! Sisi wengine tulimkatalia Rais Kikwete kwamba mgogoro wa Manispaa Bukoba haukuwa wa Amani na Kagasheki, bali Amani na madiwani waliokuwa wanapinga miradi ya kifisadi anayoisimamia.
Kama si ujasiri wa gazeti hili kuchunguza na kuandika kila mara, bila woga, hata serikali isingechukua hatua. Maana huko nyuma iliunda tume ya Abbas Kandoro ambayo ilifika Bukoba ikaona ukweli, lakini ikaufunika kwa maslahi ya kisiasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kama gazeti hili lisingekataa ujinga huu wa kisiasa na kuendelea kuibua suala hili, hata CCM taifa isingechukua hatua za kutengua uamuzi wa CCM mkoa kufukuza madiwani waliokuwa wanashinikiza meya aondoke. Tunajivunia kazi tuyliyofanya kutetea maslahi ya wananchi wa Bukoba hadi sasa.
Lakini Tanzania Daima haikuanzisha hoja hii.  Waasisi wa hoja ni madiwani wanne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika manispaa hiyo  –  Concesta Rwamlaza, Dismas Rutagwelera, Mulaki na Winfrida Mukono.
Walisema wakabezwa na madiwani wa CCM walio wengi. Lakini baadaye Mbunge wao Kagasheki alipobaini uzito wa hoja za madiwani wa Chadema, akawaunga mkono, na akashawishi madiwani wengine wa CCM kuunga mkono hoja hii kumwondoa meya.
Hapo ndipo lilijitokeza tatizo jingine. Ghafla, madiwani wawili wa Chadema – Rutagwelera na Mulaki – wakabadili msimamo, wakagoma kupiga kura ya kutokuwa na imani na meya. Wakaungwa na mkono na baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema manispaa, akiwamo mwenyekiti.
Amani akafanikiwa kuigawa Chadema Bukoba Manispaa. Akapandikiza mgogoro ndani ya Chadema. Wakaanza kutuhumiana rushwa ama ya Kagasheki au ya Amani. Mgogoro huo umedumu hadi leo, licha ya jitihada za viongozi kadhaa kutafuta suluhu.
Imekuwa fedheha kwamba hata baadhi ya viongozi wa chama kinachopiga vita ufisadi, walipopata fursa ya kumwondoa meya fisadi wakagoma kufanya hivyo. Kisingizio chao kilikuwa kile kile; eti huu ni ugomvi wa mafahari wawili – Amani na Kagasheki!
Baadhi yao, bila kujua kuwa wanaumiza Chadema, wakajikuta wakifanya kampeni za kumtengenezea Amani njia ya kuwania ubunge Bukoba Mjini, kwa kigezo kuwa wanamdhibiti Kagasheki.
Bahati nzuri, miezikadhaa iliyopita, madiwani wawili walikokuwa wamegoma kumtosa Amani waligundua kosa lao, wakarejea kundini na kushinikiza aondoke.
Naamini sasa baada ya uamuzi wa CAG hata waliokuwa wanaendekeza ujinga wa “mafahari wawili” wameona makosa yao.
Sasa ni wakati wao kuandaa mtu wa kuchukua kiti cha Amani. Wasimamie upya maendeleo ya Bukoba. Wasimamie utaratibu wa kisheria wa kumfikisha Amani mbele ya vyombo vya sheria.
Waachane na upuuzi mwingine ninaoanza kusikia sasa, eti baada ya Amani kuondoa, hawaoni mtu mwingine mwenye hadi ya kuwa meya! Huu nao ni ubozi uliopitiliza. Haustahili kukutwa Bukoba, tena Mjini.
Lakini lipo funzo la mwisho. Haya yanayotokea Bukoba Manispaa yapo nchi nzima katika halamshauri nyingi. Hili limedhihirika kwa sababu mbili. Kwanza, madiwani wa Chadema walilipigia kelele katika vikao vya Baraza la Madiwani.
Hawakusikilizwa. Wakalipigia kelele kwenye mikutano ya hadhara kwenye kata zote. Walirudia na kurudia maneno haya hadi tukayasikia.
Pili, gazeti hili la Tanzania Daima liling’ang’ania kuandika habari hizi bila woga. Wapo waliotishwa. Wapo wlaiokatishwa tama. Wapo wanaodaiwa kuhadaiwa na watuhumiwa kwa mbinu mbalimbali. Sisi tulisimama kidete; na sasa kimeeleweka.
Tulihoji nani alimruhusu Amani kukopa bilioni 4.8 kutoka Mfuko wa Dhamana? Sasa CAG amegundua kwamba milioni 200 kati ya hizo hazijulikani ziliko?
Tulihoji matengenezo ya barabara ya ya thamani ya Sh 138 bilioni; ambayo sasa CAG amegundua kumbe zilitumika Sh 227 bilioni, bila nyaraka halisi, na bila idhini ya mkandarasui wa serikali.
Tulihoji nani aliidhinisha Sh 789 milioni za ujenzi wa soko jipya. Tulihoji kwanini Manispaa imekataa kukusanya mapato ya Sh. 256 milioni kwa jeuri ya Amani. Tulihoji hatima ya wamiliki wa viwanja 800 na kadhalika.
Hatukuhoji dini ya mtu wala uraia wake. Haya ndiyo yalipaswa kupatiwa majibu mapema. Na ndiyo yatamwingiza Amani matatani.
Swali muhimu. Haya ya Bukoba yamejulikana. Je, kwingine kuko salama?

1 comment:

  1. HILI NALO LITAPITA
    SI SI SWALA LA AMANI WALA KAGASHEKI WATANZANIA TUNATUMIAJE HAKI YETU YA KUHOJI MAPATO NA MATUMIZI KATIKA NGAZI TULIZOMO YA MANI YAKWISHA LAKINI BUKOBA IPO NA ITAENDELEA KUWEPO HATA BILA KAGASHEKI YA MSINGI NI HAYA KWA MAONI YANGU:
    1:KAMA WEWE NI MWANACHAMA WA CCM KATIBA INASEMAnanukuu baadhi ya maneno "NITASEMA KWELI DAIMA FITINA KWANGU MWIKO"misho wa kunukuu. ANGALIA LA UONGO NA FITINA LIMEIFIKISHA WAPI BUKOBA NA LINAIPELEKA WAPI TANZANIA KWA UJUMLA ?
    2:KAMA WEWE NI MWANACHAMA WA CHAMA CHOCHOTE CHA UPINZANI KAM MTANZANIA KATIBA YA SASA YA JAMHURI YA MUUNGANO INAKUHITAJI KULINDA KUTETEA NCHI KWA WELEDI,AKILI, NA MAARIFA ULIYO NAYO KWA MANUFAA YA KIZAZI KICHACHO.+JE UMEFANYA HIVYO?
    3:UDINI,UKABILA NA UBAGUZI NI HULKA YA WATU WA BUKOBA HASA MNAOISHI HIVI SASA HAPA MJINI BUKOBA NA HILI NI JANGA KUBWA NDO LINPELEKEKA YOTE HAYA YANATOKEA BUKOBA KWA KIUULIZANA KATOKA WAPI HUYU "oli wa nka" .
    4.MAKUNDI YA USHABIKI WA KIHOLELA ISIOKUWA NA TIJA NDANI NA NJE YA VYAMA, NA HASWA KATIKA JAMII IZUNGUKAYO VIUNGA VYA MJI WA BUKOBA LIMEKITHIRI SANA NALO NI TATIZO KUBWA KWA WAKAZI WA MJI HUU.
    5.MAKUNDI YA VIJANA TEGEMEZI NDIYO YANAYOENEZA CHUKI,UONGO,UZANDIKI,UMBEA,UNAFIKI NA AINA KAMA HIZO AMABZO SIKUZITAJA KWA KUFADHILIWA NA VIONGOZI WA KISIASA NALO NI TATAIZO.
    HITIMISHO
    BUKOBA NI MJI MKONGWESANA ILA HAUJAENDELEA SANA NA HAUNA MAENDELEA NA HAUTAPATA MAENDELEO HADI PALE UJUAJI,UBINFSI,SIASA ZA CHUKI NA UROPOKAJI VITAKAPO KWISHA KWA WANABUKOBA KUJIKANA WENYEWE KATIKA NAFSI ZAO NA KUTAMBUA MJI WA BUKOBA ULIKUWEPO NA UTAKUWEPO BILA KAGASHEKI AU AMANI AMA MWINGINEWE YEYOTE ANAEJISIKIA BILA YEYE BUKOBA HAIPO.

    ReplyDelete