Mbunge
wa Nzega, Dk Khamis Kigwangalla, (CCM), leo anatarajiwa kuanza
kukusanya saini za wabunge akitafuta kuungwa mkono katika hoja ya
kutokuwa na imani na Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa madai kwamba
amekuwa akikiuka kanuni za Bunge.
Dk
Kigwangalla aliibua hoja ya kutokuwa na imani na Spika katika kikao cha
wabunge wote cha kuelezea shughuli zitakazofanywa na Bunge katika
mkutano wa 13, kilichofanyika juzi jioni kwenye ukumbi wa Pius Msekwa.
Mbunge
huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, jana alithibitisha kuwapo kwa mjadala huo katika
kikao cha wabunge, lakini hakuwa tayari kueleza kwa undani na badala
yake alisema kwamba leo ataanza kukusanya saini za wabunge kwa ajili ya
kukamilisha hoja ya kutokuwa na imani na Spika Makinda.
Chanzo
chetu kutoka katika kikao hicho cha wabunge kilibainisha kuwa
Kigwangalla alihoji kuhusiana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Bajeti, Andrew Chenge (CCM-Bariadi Magharibi) kuteuliwa na Spika wakati
katika kamati nyingine wenyeviti na makamu huchaguliwa na wajumbe wa
kamati husika.
Pia
Dk Kigwangala alisema Spika Makinda alivunja kanuni kwa kuwapa posho ya
Sh430,000 kwa siku wajumbe wa kamati inayoongozwa na Chenge wakati
wajumbe wa kamati nyingine wamekuwa wakipewa Sh130,000.
“Anachokifanya
Spika ni matumizi mabaya ya fedha za umma, inakuwaje wengine wafanye
kazi hata bila posho lakini wao (Kamati ya Bajeti), walipwe posho ya
Sh430,000 kwa siku?” chanzo hicho kilimkariri Dk Kigwangalla akihoji.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah akizungumza na gazeti
hili jana alisema mazingira ya kamati fulani kupata malipo ya ziada
tofauti na viwango vya kawaida hutokea pale uongozi wa kamati husika
unapoomba kwa Spika.
“Si
kweli kwamba Kamati ya Bajeti inalipwa fedha za ziada kila wakati,
hapana, ni pale tu wanapoomba malipo hayo kutokana na sababu ambazo
lazima Spika aridhike nazo. Ieleweke kuwa siyo kamati hiyo tu, kwa sasa
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ambayo inachambua miswada mingi nayo
imekuwa ikiomba na baada ya Spika kuridhia basi nao wanapewa,” alisema
Dk Kashililah.
Katibu
huyo wa Bunge alieleza kuwa zaidi ya kamati nane zimewahi kuomba malipo
ya ziada kwa maana ya kutaka posho zaidi, ulinzi, usafiri na hata
chakula, ikiwa zinakabiliwa na majukumu ya ziada pia katika mazingira
tofauti nje ya utaratibu wa kawaida.
“Kimsingi,
kamati nyingi zinapewa malipo tofauti, watu wanaweza kuwa na kazi mpaka
saa saba au nane usiku, au wanakwenda kufanya kazi katika mazingira
yasiyokuwa ya kawaida, taratibu zinamruhusu Spika kama akiridhika na
maelezo ya kazi husika, basi anaruhusu kutekelezwa kwa maombi hayo,”
alisema Dk Kashililah.
Kuhusu Serukamba
Aidha,
Dk Kigwangalla alinukuliwa akisema Spika amekiuka kanuni kwa kumchagua
Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Peter Serukamba (Kigoma Mjini-CCM),
kuwa mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti.
No comments:
Post a Comment