Monday, 28 October 2013

HOTUBA YA KWANZA YA JAMAL MALINZI,RAISI MPYA WA TFF


 Hatimaye Tumechagua Mabadiliko,
Salamu kwa wanafamilia wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Salamu kwa wapenda michezo wa ndani na nje ya nchi yetu Tanzania.

Naanza kwa kumshukuru Mungu kwa hekima, busara, akili, vipaji na uwezo aliotujaalia kutuwezesha kutenda yote haya kwa amani na utulivu.

Shukrani za dhati zimwendee Bw. Leodegar Tenga, rais wa TFF 2005 - 2013 anayekabidhi madaraka kwa rais mpya wa TFF. Yeye na timu yake kwa hakika wanastahili pongezi kwa mengi mazuri waliyofanya.

Shukrani kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi 2013 kwa kunikubali, mimi Jamal E. Malinzi niwe Rais wa TFF kwa kipindi kijacho cha miaka minne.

Kweli dunia imekuwa kijiji, kwani kipindi cha masaa 72 baada ya kuzindua ilani yangu ya uchaguzi, nimepokea salamu, maoni na mapendekezo toka ndani na nje ya Tanzania ikiwa ni pamoja na Burundi, Ivory Coast, Denmark na NewZealand.

Kupitia www.jamalmalinzi.com, twitter @jamalmalinzi, Jamii Forum, Facebook na mitandao mingine, naomba tuendelee kuwasiliana, kutoa maoni, kukosoa na kuchangia mijadala yenye tija na ufanisi ili Tanzania yote ipate neema ya mpira wa miguu.

Safari ni ndefu na wasafiri ni wengi kwenye vyombo vichache vya usafiri. Kwa wale ambao tayari wana ramani ya safari yetu, sote bila kujali tofauti zetu hasa wakati wa kuwania uongozi, tutoe mchango wake ili Tanzania isonge mbele katika ulimwengu wa soka.

Naam, kuna msemo wa Kiswahili unaosema 'kukata tamaa ukingali unaishi ni dhambi'. Naomba msemo huu na utuongoze kila tunapojikwaa tunanyuke na kuendelea na safari hadi tufike tulipopakusudia.

Historia imeshaanza kuandikwa, mwaka 2013 ni Tumechagua Malinzi, Tumechagua Mabadiliko na sasa tunasonga mbele.
Jamal E. Malinzi
Oktoba 27, 2013

No comments:

Post a Comment