Wednesday, 4 September 2013

Mnigeria adakwa na dawa za kulevya Dar es Salaam



“Baada ya kumhoji ametueleza kuwa dawa hizo alizinunua maeneo ya Magomeni, kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi na mahojiano zaidi.” Clemence Jingu 
Kwa ufupi
  • Kete hazijajulikana ni za aina gani, kwa sasa tunafanyika utaratibu wa kutambua aina yake.



Dar es Salaam. Mwanamke ambaye ni raia wa Nigeria, amekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), akiwa na kete 99 za dawa za kulevya.
Hata hivyo kete hizo hazikujulikana ni za aina gani.
Kukamatwa kwa raia huyo, kumekuja wiki tatu tangu Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, kutangaza vita dhidi ya watu wanaopitisha dawa za kulevya katika idara na taasisi zilizoko chini ya wizara yake.
Akizungumza na Mwananchi jana, Meneja Usalama wa uwanja huo, Clemence Jingu, alisema mtuhumiwa alikamatwa jana saa 8:00 mchana
Alisema kete hizo alikuwa ameziweka katika makopo ya poda na mafuta.
“Kete hazijajulikana ni za aina gani, kwa sasa tunafanyika utaratibu wa kutambua aina yake,” alisema.
“Kwa sasa hapa JNIA kuna mitambo ya kisasa ya kuweza kuwabaini wanaopitisha dawa hizi, tulimkamata akiwa na kete 99, kati ya hizo kete 30 alikuwa ameweka katika kopo la mafuta ya nywele, kete nyingine alikuwa ameweka katika kopo la poda za watoto,” alisema.
Alisema kuwa raia huyo wa Nigeria alikuwa akielekea Roma, Italia kupitia Paris, Ufaransa kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia.
“Baada ya kumhoji ametueleza kuwa dawa hizo alizinunua maeneo ya Magomeni, kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi na mahojiano zaidi,” alisema.
Alisema kuwa binti huyo aliingia nchini Agosti 30mwaka huu, akitokea nchini Nigeria.

No comments:

Post a Comment