Tuesday 3 September 2013

MJADALA wa Bunge jana jioni ulitawaliwa na kauli nzito baada ya wabunge kadhaa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kutuhumiana kuhusika na ubadhirifu katika vyama vya ushirika nchini.

Hoja hiyo iliibuka wakati Bunge likijadili muswada wa sheria ya vyama vya ushirika wa mwaka 2013 uliowasilishwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Balozi Christopher Chiza.
Aliyekuwa wa kwanza kuwasha moto huo baada ya mapumziko ya mchana alikuwa mbunge wa Busega, Dk.Titus Kamati (CCM), ambaye alisema waziwazi kuwa wanasiasa ndio wezi wa vyama vya ushirika.
Dk. Kamani alihoji ni kwa nini serikali inapata kigugumizi kuwachukulia hatua wahusika na kusisitiza kuwa hapo kuna kulegalega kumaliza ufisadi katika ushirika.
“Wanasiasa hawa kwa nafasi zao wameingia kwenye ushirika na kufanya ufisadi lakini serikali inashindwa kuwachukulia hatua.
“Huku ni kulegalega na ndio maana hata tumeshindwa kuwataja wauza dawa za kulevya, waziri anaishia kusema tunayo orodha,” alisema.
Alihoji ni kwa nini sasa serikali isiige mfano wa China wa kuwafunga na hata ikibidi kuwanyonga watuhumiwa wa ufisadi wa vyama hivyo ikithibitika bila kujali nafasi zao kwenye siasa.
Mbunge wa Mpanda Vijijini, Moshi Kakoso (CCM), ndiye aliyefuata na kuchafua hali ya hewa kwa kumtuhumu Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Nchini (TTB) kufanya ufisadi mkubwa ambao serikali inaujua lakini imeamua kuunyamazia.
Bila kumtaja kwa jina lakini alikuwa akimlenga mbunge mwenzake wa Namtumbo, Vita Kawawa, akisema kuwa anajilipa mshahara mara mbili ya ule uliopitishwa na serikali.
Alisema kuwa analipwa sh milioni mbili za mawasiliano na anachukua dola 1200 (zaidi ya sh milioni 1.8) kwa ajili nyumba badala ya sh 800,000 zilizoidhinishwa.
Mbunge huyo alisema mwenyekiti huyo anayajua mambo hayo na ndiye aliyeidhinisha.
“Nina uhakika na ninachozungumza, waziri nilishamletea taarifa juu ya jambo hili lakini amenyamaza, hivi hapa tunategemea ushirika utakuwa hai wakati mabosi wanautafuna?” alihoji.
Wakati mbunge huyo anaendelea kuzungumza, Kawawa akitaka kumpa taarifa juu ya jambo analolizungumza.
Kawawa alisema muda wake wa kuwa mwenyekiti kwenye bodi hiyo uliisha Juni 31 mwaka huu, hivyo ni vema mbunge mwenzake akatoa ushahidi wake juu ya tuhuma za watendaji wa bodi husika.
Baada ya Kawawa kumaliza, Kakosa aliendelea kuchangia ambapo alikataa taarifa hiyo kwa madai ana ushahidi wa kile kilichofanyika.
Mara baada ya Kakoso kumaliza kuchangia muswada huo, mbunge wa Kondoa Juma Nkamia alipewa fursa ya kutoa taarifa ambapo alisema tuhuma zilizotolewa na Kakoso dhidi ya Kawawa ni nzito sana na Bunge lipate fursa ya kuangalia jambo hilo pamoja na mhusika kutoa ushahidi.
Naibu Spika, Job Ndugai, alisema ofisi ya Bunge iko wazi kwa Kakoso kuwasilisha ushahidi wake juu ya kile alichosema.
Mara baada ya Ndugai kutoa ufafanuzi huo, alimpa nafasi mbunge wa Sikonge, Saidi Nkumba (CCM), ambaye alimtuhumu Kakoso kwa kushindwa kuliambia ukweli Bunge kuwa yeye ni Mwenyekiti wa Chama Kilele (APEX) ambacho kinapigiwa kelele kuwa kinawanyonya wakulima.
Alisema wakiwa Dar es Salaam kwenye vikao vya kamati za Bunge, Katibu wa Apex, aliitwa katika kamati kama mdau ambapo alipobanwa juu ya wizi unaofanyika kwenye chombo hicho alisema serikalini ikiiba kelele zinapigwa lakini APEX ikiiba kidogo kelele zinakuwa kubwa sana.
“Katibu wa Kakoso ndiye aliyetuambia hivyo. Huu ni wizi, sisi hatuwezi kukubaliana na jambo hilo, serikali haivumilii wizi, huyu Kakoso anasema APEX ni mkombozi lakini pale Tabora wamewaibia wananchi bilioni 16, hivi kweli hizi si fedha nyingi?
“Hii APEX ni lazima ifutwe, wenye tamaa ya kwenda kwenye ushirika ni vema waache siasa, na wenye ushirika ni vema wakabaki huko huko.”
Alibainisha kuwa wizi unaofanyika kwenye vyama vya ushirika unasababishwa na wanasiasa ambao wana kinga za kisiasa ndiyo maana wanaendelea kutafuna fedha za wananchi.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali, alisema wabunge wana taarifa za wizi wanatoa taarifa hapa bungeni lakini hakuna wanachokifanya.
“Yaani kila kukicha mnalea wizi halafu leo hii mnaanzisha tume za kuwanyonya wakulima, kule kwangu wakulima waliuza tumbaku, msianzishe vitu vya ajabu ajabu…, huu ni wizi mtu, msituletee wizi hapa kwa kubadilisha majina ya vitu,” alisema.
Tundu Lissu wa Singida Mashariki (CHADEMA) alisema sababu kubwa ya kuporomoka kwa ushirika ni serikali kuuingilia, kuudhibiti na kuuporomosha.
Alisema serikali ilianza kuvuruga mambo 1966 sheria za ushirika ilibadilishwa na msajili wa vyama vya ushirika alipewa mamlaka ambayo alianza kuyatumia vibaya ambapo mwaka 1976 alipigwa marufuku zikaja bodi za mazao.
Mwaka 1982 vilirejeshwa vyama vya ushirika lakini mamlaka yake yalikuwa yakitolewa na mrajis ambaye ni serikali.
Mbunge wa Nzenga, Andrew Kigwangalah, aliibua upya mzozo wa awali kwa kuanika nyaraka za ufisadi katika TTB kama ilivyokuwa imedokezwa awali na Kakoso.
Kingwangalah ambaye alidai kuwa hatarudi nyuma kuwataja mafisadi na wauza dawa za kulevya alisema kuwa kodi ya nyumba ya mwenyekiti wa bodi inalipiwa gahara tofauti na ile iliyoidhinishwa.
Alionyesha nyaraka kadhaa za malipo ya viongozi wa bodi hiyo na kisha kumvaa Nkumba akisema kuwa tatatizo la nchi hii si Apex bali ni rushwa, wizi, ubadhirifu halafu watu wanaona wizi wanaungalia badala ya kuchukua hatua.
“Waliobaki kwenye ushirika ni wezi watupu, wazalendo wameisha, wezi tunawajua lakini hatuwawajibishi wala kuwachukulia hatua.
“Nkumba ni msaidizi wa Kawawa katika bodi ya tumbaku anajua ukaguzi haujafanyika na ukifanyika wao hawatasalimika ndiyo maana wanaanza kuipiga vita Apex.
“Kuna watu wanatumiwa na kampuni za ubebari ambazo zilikuwa zikisafirisha tumbaku na kusambaza pembejeo, hawa sasa wanaona hatari za kampuni zao ndiyo maana zinawatumia wabunge ili APEX ifutwe, tuwe makini na wabunge waovu,” alisema.
Mzozo huo ulidumu huku Kawawa na Nkumba wakisimama kujitetea bila mafanikio hatua iliyomlazimu Naibu Spika wa Bunge kutoa nafasi kwa baadhi ya wabunge kuomba viongozi, lakini akaliahirisha Bunge hadi leo ambapo atatoa uamuzi wake.
Mapema asubuhi, wabunge walipendekeza wabadhirifu wa mali za ushirika walazimishwe kufidia hasara iliyotokea pamoja na kufilisiwa mali zao.
Pendekezo hilo limetolewa na Nkumba alipokuwa akisoma hotuba ya Mwenyekiti wa 
Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Peter Msolla.
Nkumba alisema ushirika umewakatisha tamaa wananchi kutokana na ubadhirifu wa viongozi wake hivyo ujio wa sheria hiyo utakuwa mkombozi.
Aliongeza kuwa watuhumiwa wa ubadhirifu wa ushirika wafikishwapo mahakamani mashauri yake yamekuwa hayathibitiki licha ya taarifa za fedha kuonyesha kuwa upotevu fedha upo; ni vema kuwepo na utaratibu wa kuwabana wahusika.
Nkumba alisema vyama vya ushirika vimekuwa vikikaguliwa na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (Coasco) ambalo halifanyi kazi zake vizuri na kuitaka serikali kuweka utaratibu mzuri ikiwemo kuhusishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali.
Waziri wa Kilimo, Chiza alisema kuundwa kwa sheria hiyo litakuwa suluhisho la matatizo ya ushirika nchini.
Alisema serikali inalenga kuifuta sheria ya vyama vya ushirika namba 20 ya mwaka 2003 na inaamini sheria mpya itaimarisha, kuendeleza na kuufufua ushirika.
Chiza alisema sheria ya ushirika ya mwaka 2013 ina lengo la kutekeleza sera ya maendeleo ya ushirika ya mwaka 2002, inayovitaka  vyama vya ushirika imara, endelevu na vyenye kukidhi mahitaji ya wanachama kiuchumi chini ya mazingira ya soko huria.

No comments:

Post a Comment