Thursday 14 May 2015

WAZIRI WA AFYA AIPONGEZA MUHIMBILI KUFANIKISHA MATIBABU YA MOYO KWA WATANZANIA

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mh. Dkt. Seif Rashid ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia Idara yake ya Tiba na Upasuaji Moyo kwa kufanikisha matibabu ya moyo kwa wagonjwa 24 katika kipindi cha siku nne.
Hayo ameyasema alipotembelea Hospitali hiyo kuona namna ambavyo wataalam wetu kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Prince Sultan Cardiac Centre iliyoko Riyadhi nchini Saudi Arabia ambao wamekuwepo Muhimbili toka tarehe 9 Mei na wanatarajiwa kuondoka tarehe16 Mei, mwaka huu.
Dkt. Rashid amesema ni mfanikio makubwa sana ambayo tumefikiwa hadi hivi sasa katika upasuaji moyo na tunatarajia kasi hii ya ushirikiano ikiendelea tutapunguza kwa kasi sana wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

“Kama ndani ya siku nne tu mmeweza kuziba matundu ya moyo kwa watoto 12 bila kufungua kifua na mkaweza kufungua vifua vya watoto wengine 12 ambao kutokana na hali zao walihitaji kufunguliwa vifua, mmenipa moyo sana kwamba mmejidhatiti kuhakikisha Watanzania wanapata huduma hii kwa haraka na kwa ufanisi wa hali ya juu, nawapongezeni sana” amesema Dkt. Rashid.


Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid akiwa na mtoto ambaye anasubiri kufanyiwa uchunguzi wa kina kama anahitaji upasuaji wa moyo au la.

mtoto Catherine Gwabala (6) alikuwa wodini jumamosi iliyopita akisubiri kufanyiwa upasuaji.

Mh. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid akimjulia hali leo baada ya kufanyiwa upasuaji. Kushoto kwake ni mama Catherine akifurahia baada ya mtoto wake kufanyiwa upasuaji.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashid ambapo kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Hussein Kidanto wakiwa ndani ya Chumba chenye mtambo wa Cath Lab ambao unatumika kuzibua mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye moyo iliyoziba na pia mtambo huu pamoja na mambo mengine umetumika kwa mara ya kwanza kuziba matundu ya moyo bila kufungua kifua. Mtoto huyu ambaye jina lake limehifadhiwa anasubiri kuzibwa tundu kwenye moyo wake kwa kutumia mtambo wa Cath Lab. Ndani ya siku tatu ataruhusiwa kwenda nyumbani.

Hapa ni ndani ya chumba chenye vifaa vya kisasa kabisa kwa ajili ya wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU) ambapo mtoto aliyefanyiwa upasuaji anaangaliwa.

Jopo la wataalam wakiwa ndani ya chumba cha kisasa cha upasuaji moyo wakiendelea na upasuaji moyo.

Jopo la Watalaam wakifurahi baada ya kumaliza upasuaji kwa ufanisi na mgonjwa kupelekwa chumba maalumu (ICU).

Mtoto Cherish Chatama akifurahi baada kusalimiwa na Mh. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid ambapo pembeni yake ni mama Cherish

Mtoto Michelle Colila (5) akifurahi baada kusalimiwa na Mh. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid ambapo pembeni yake ni mama Michelle.

No comments:

Post a Comment