- Waziri mkuu pia alisema eneo hilo lililotengwa kwa uhifadhi ndilo tegemeo la wananchi kwa ajili ya malisho ya mifugo hasa nyakati za kiangazi, pia kuna makazi ya watu, shule na huduma nyingine muhimu.
Loliondo. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ametengua
tangazo la Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki la
kuligawa eneo la Pori Tengefu la Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro, mkoani
Arusha kwa kutenga kilomita za mraba 1,500 kwa ajili ya uhifadhi na
kilomita za mraba 2,500 kuwa chini ya Serikali za vijiji.
Machi 19, mwaka huu, Waziri Kagasheki alitoa
tangazo la Serikali la kuligawa pori hilo lenye ukubwa wa kilomita za
mraba 4,000 ili Serikali iweze kuhifadhi eneo la kilomita za mraba 1,500
ambalo alieleza kuwa ni mapito na mazalia ya wanyamapori, pia kutunza
ikolojia ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Tangazo hilo liliibua mgogoro
mkubwa.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika eneo
la Waso jana baada ya kutembelea eneo la mgogoro na kufanya kikao na
ujumbe wa mawaziri alioambatana nao na watendaji wa wizara mbalimbali,
Waziri Mkuu alisema amefikia uamuzi wa kuondoa tangazo hilo la Serikali
na sasa wananchi wa eneo hilo wataendelea na utaratibu uliozoeleka.
Mawaziri waliokuwa katika ziara hiyo ni Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi,
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa
Maji, Dk Binilith Mahenge, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,
Benedict Ole Nangoro na Naibu Waziri (Tamisemi), Kassim Majaliwa.
“Mara baada ya lile tangazo kuliibuka mgogoro wa
wananchi kupinga na baadhi ya viongozi walinifuata hadi Dodoma na
kuniletea malalamiko yao. Pia CCM iliunda tume na kunipa taarifa lakini
nikasema siwezi kutoa uamuzi hadi nifike mwenyewe katika eneo hili na
sasa nakubaliana na hoja za wananchi kuwa kuligawa eneo kutakuwa na
athari kwenu, naomba sasa mwendelee na utaratibu wenu kama vile
halikuwepo tangazo hilo,” alisema Pinda.
Alisema miongoni mwa hoja za wananchi
zilizosababisha afikie uamuzi huo, ni kuwa eneo hilo la kilomita za
mraba 1,500 ndilo ambalo lina vyanzo vya maji vinavyotegemewa na vijiji
vyote sita ambavyo vingeathiriwa na tangazo hilo. Vijiji hivyo ni
Ololosokwani, Soitsambu, Olorieni Magaiduru, Arash, Piyaya na Oloipili.
Waziri mkuu pia alisema eneo hilo lililotengwa kwa
uhifadhi ndilo tegemeo la wananchi kwa ajili ya malisho ya mifugo hasa
nyakati za kiangazi, pia kuna makazi ya watu, shule na huduma nyingine
muhimu.
Alisema kutokana na uamuzi huo, Serikali
inajipanga kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika wilaya hiyo
ili kutambulika maeneo ya ufugaji, makazi, kilimo na uhifadhi ili
masilahi ya kila upande yaendelee kulindwa.
“Utaratibu wenu mliojiwekea kabla ya tangazo la
Serikali uendelee kwani tunataka shughuli za uwindaji wa kitalii
ziendelee, upigaji picha uendelee, pia ufugaji uendelee na hapa ni vyema
kukawa na vikao vya wadau wote walau kila baada ya miezi mitatu,”
alisema Pinda.
Waziri Mkuu aliagiza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Arusha na Halmashauri ya Ngorongoro kuratibu vikao hivyo kwani lengo ni
kutatua migogoro na kurejesha uhusiano.
No comments:
Post a Comment