Tuesday 15 March 2016

KAMISHNA WA JESHI LA POLISI ZANZIBAR AZUNGUMZIA JUU YA MIRIPUKO INAYOTOKEA UNGUJA NA PEMBA.


Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu matokeo ya uripuaji wa mabomu na kuchoma moto nyumba na maskani za CCM Unguja na Pemba. Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.

Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame leo Zanzibar.
Na Mwashungi Tahir na miza Kona - Maelezo Zanzibar 15/03/2016
NYUMBA ya Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame imeripuliwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu na watu wasiojulikana majira ya saa 5.00 usiku huko Kijichi nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Ofisini kwake Makao Makuu ya Polisi Kilimani, Kamishna Hamdani amesema tukio hilo limeathiri sehemu ya paa la nyumba na dari na kujeruhi baadhi ya watu waliokuwa wamelala na kusababisha hasara kubwa.

Amesema tukio hilo linafanana lile lililotokea tarehe 03 mwezi huu katika Maskani ya CCM Kisonge Unguja hivyo polisi inaendelea kufanya uchunguzi ikiwa ni pamoja na kuwasaka wahalifu wanaofanya uhalifu huo.
Akizungumzia matukio mengine ya uhalifu na kuchoma moto nyumba, maskani na kituo cha Afya huko Pemba, alisema Jeshi la Polisi limeanza msako mkali na kuwatia mbaroni watu 31 ambao wanaendelea kuhojiwa na watakaohusika watafikishwa katika vyombo vya sheria.

Kamishna Hamdani amewatowa hofu wananchi kuhusu usalama wao na mali zao kuelekea uchaguzi wa marudio utakaofanyika tarehe 20 mwezi huu na kuwepo kwa ongezeko la askari katika maeneo mengi ya mijini na vijijini ni moja ya juhudi za kuimarisha ulinzi na kuhakikisha uchaguzi huo utakuwa salama na amani.

Ametahadharisha kuwa mtu yoyote atakayejihusisha kuanziasha vurugu au kufanya kitendo chenye ishara ya uvunjifu wa amani atapambambana na vyombo vya sheria.

Kamishna Hamdani ametowa wito kwa wananchi waliojiandikisha kupiga kura kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili waweze kutimiza haki yao ya msingi ya kikatiba bila ya woga kwani jeshi hilo limejipanga kuimarisha ulinzi sehemu sehemu zote.

No comments:

Post a Comment