MKUU wa Mkoa (RC) wa Kagera, Kanali mstaafu Fabiani Massawe,
anafanya mbinu za kutaka kupindisha ukweli kuhusu tuhuma zinazomkabili
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani.
Manispaa hiyo imekumbwa na mgogoro mkubwa kati ya madiwani na meya
huyo, vikao vya madiwani havikutani kwa zaidi ya mwaka. Suluhu
imeshindikana hadi kufikia hatua ya kuletwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ili akague miradi
inayolalamikiwa.
Wakati ripoti ya CAG ikisubiriwa iseme kilichobainika, mkuu wa mkoa
anajaribu kutumia njia za panya kutaka kumaliza mgogoro huo kwa mbinu
za kijanja.
Huku akielewa wazi kwamba madiwani wamechaguliwa na wananchi na hivyo
wanawajibika kwao, Massawe anaamua kuitisha kikao alichokiita cha
usuluhishi ili kuwashawishi wakubali kuketi na ‘mtuhumiwa’ kupitisha
bajeti ya 2014/2015.
Massawe anajificha kwenye migongo ya viongozi wa dini, Askofu
msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini, Sheikh wa
Wilaya ya Bukoba, Haruna Kichwabuta na wazee maarufu ili wamsaidie
kuwalainisha madiwani, lakini anagonga mwamba.
Madiwani hao wanane wa CCM wanaompinga meya pamoja na wale saba wa
upinzani, wanamshangaa Massawe na viongozi wake wa usuluhishi kuwa
walikuwa wapi mwaka mzima wakati mgogoro huo ukiendelea.
Wanahoji kwanini asubiri hadi ripoti ya CAG inakaribia kuletwa mezani
ndipo anazunguka kuwalainisha ili wapitishe bajeti upesi, tena kwa
vitisho na ubabe kwamba watakaogoma kuhudhuria watafukuzwa udiwani.
Tunahoji kwa Massawe tukitaka kufahamu hasa analenga kuficha nini
katika mgogoro huo wa Bukoba. Kwanini awe na haraka wakati ripoti ya CAG
yenye ukweli wote iko tayari?
Kama naye sio sehemu ya ufisadi huo, ni kwanini asingoje CAG
aiwasilishe ripoti ili isomwe na mchawi wa maendeleo ya Bukoba ajulikane
kama ni madiwani au meya na viongozi wa serikali?
Mgororo wa Bukoba haukuanza juzi wala jana, viongozi wa dini pamoja
na hao wazee wanaojaribu kutumiwa na Massawe, lazima watiliwe shaka
kwamba walikuwa wapi tangu viongozi wote wa juu wa CCM akiwemo Rais
Jakaya Kikwete wanashindwa kuutatua hadi kuomba CAG awatafutie ukweli?
Sasa kama ukweli huo uko tayari, kwanini Masaswe anajaribu kuzunguka
mlango wa nyuma ili wananchi wasijue CAG alibaini nini? Katika jitihadi
hizi za udalali wa kujaribu kumkinga Meya Amani, mkuu wa mkoa ana
maslahi gani?
Kwa kitendo alichokifanya Massawe juzi, ni wazi kuwa amewadharau
viongozi wa CCM na mkuu wake, yaani Rais Kikwete kwa kuingilia suala
ambalo uamuzi wake ulikwishapelekwa kwenye ngazi nyingine.
Massawe ameletwa kuiongoza Kagera kama mteule na ataiacha wakati
wowote mteule wake atakapoamua vinginevyo, sasa ni kwanini hawapi
nafasi wawakilishi halali wa wananchi (madiwani) wakatimiza majukumu
yao kwa kuzingatia utaratibu unaofaa?
No comments:
Post a Comment