Tuesday 14 January 2014

RC AMTUMIA KILAINI KUMNASUA MEYA BUKOBA

Kanali mstaafu Fabian Massawe na  Meya wa  Bukoba, Anatory AmaniMKUU wa Mkoa (RC) wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe, amekimbilia kwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini, Sheikh wa Wilaya, Haruna Kichwabuta na wazee maarufu ili wamsaidie kumnasua Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani, asing’olewe na madiwani.
Hatua hiyo inakuja wakati ambapo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Uttouh, akitarajiwa kuwasilisha ripoti ya ukaguzi wa miradi ya kifisadi katika manispaa hiyo wakati wowote.
Amani aliingia kwenye mgogoro na madiwani wake wakiwemo wanane wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki na wenzao saba wa CHADEMA na CUF wakitaka kumwondoa kutokana na tuhuma za kuendesha miradi ya kifisadi.
Baada ya mgogoro huo kuwa mkubwa na CCM ngazi ya taifa kushindwa kuumaliza, hatimaye Kamati Kuu ya chama hicho ilimwomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kupitia Wizara ya Tamisemi kufanya ukaguzi maalumu wa tuhuma hizo kupitia kwa CAG.
Oktoba 10, mwaka jana, CAG alianza ukaguzi huo na tayari amekamilisha ripoti yake akisubiri kuikabidhi, lakini kumekuwa na juhudi za makusudi za kutaka kuipotosha taarifa hiyo ili isiwasilishwe kwa madiwani.
Mkuu wa Mkoa ambaye amekuwa mtetezi mkubwa wa Meya Amani, jana aliitisha kikao cha dharura kati yake na madiwani wanane wa CCM wanaompinga Amani na kuwalainisha waondoe tofauti zao ili Baraza la Madiwani lianze vikao vyake.
Wakizungumza na gazeti hili kwa simu jana kutoka mjini Bukoba, baadhi ya madiwani hao walieleza kushangazwa na kitendo hicho cha Massawe ilhali wanasubiri ripoti ya CAG iwasilishwe ili wajue kile kilichobainishwa kwenye uchunguzi.
“Sisi tumemuuliza mkuu wa mkoa, wakati mgogoro huo ukiendelea hadi leo ambapo vikao havifanyiki, hao viongozi wa dini na wazee walikuwa wapi kutafuta muafaka hadi wangoje CAG amalize ukaguzi na ripoti inakaribia kutolewa ndipo waje kutusuluhisha?
“Kwanza, kama tungekubali huo mtego wao wananchi wetu wangetushangaa na kamwe wasingetuelewa kuona kile tulichokipigania kinakaribia kutolewa hadharani kujua ukweli halafu tunageuka,” alisema mmoja wao.
Tanzania Daima lilidokezwa kuwa Massawe alijaribu kuwasihi madiwani hao bila mafanikio akidai kuwa ripoti ya CAG haipo na kwamba kama itakuwepo huenda ikachelewa kwa muda wa miezi miwili, hivyo kuwataka waingie kwenye vikao vya baraza kupitisha bajeti.
“Baada ya kuona tumeshikilia msimamo wetu, Massawe alitumia ubabe kumwagiza Katibu Tawala aitishe vikao hivyo kwa nguvu ili tutakao kaidi tuchukuliwe hatua za kinidhamu za kuwajibishwa.
“Sasa tumemtaka atueleze kama yeye yuko juu ya Rais Jakaya Kikwete, maana baada ya yeye kushindwa kumaliza mgogoro wetu ndipo kupitia kwa Waziri Mkuu alimwagiza CAG aje kukagua. Sisi tumemwambia kwamba tunataka ripoti zote ile ya Abbas Kandoro na CAG na si vinginevyo,” alisema diwani mwingine.
Kikao cha jana kilihudhuriwa na Alexander Ngalinda wa Kata ya (Buhembe), ambaye pia ni Naibu Meya, Yusuf Ngaiza (Kashai), ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendagulo), Richard Gaspar (Miembeni) na Murungi Kichwabuta wa Viti Maalumu.
Balozi Kagasheki na Dauda Kalumuna (Ijuganyondo) hawakuweza kuhudhuria kikao hicho kutokana na kuwa katika majukumu  mengine.
Miradi iliyokuwa inalalamikiwa ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhama ya Uwekezaji (UTT) haukufuata taratibu, na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo.
Ipo pia ujenzi wa soko ambapo meya anadaiwa kusitisha malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata utaratibu.
Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Uwekezaji (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani. Vile vile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90, lakini hakueleza misingi yake.
Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh milioni 297 zinazotiliwa shaka. Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya mradi kiasi cha sh milioni 134, za ujenzi wa kituo cha mabasi.

No comments:

Post a Comment