- Alisema walipofika katika eneo hilo walikuta makontena mawili, moja lilikuwa limejaa samaki ambao walionekana kuwa wazima huku lile lililokuwa nusu lilikuwa na samaki walioharibika kutokana na kutoa harufu na kuzingirwa na inzi.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Chakula na Dawa
Tanzania (TFDA), imekamata kilo 7,500 za samaki aina ya vibua
walioharibika ambao waliagizwa na Kampuni ya Sais Boutique kutoka China,
Julai mwaka huu.
Taarifa ya kuwapo kwa samaki hao sokoni
iliripotiwa na Gazeti la Mwananchi Jumapili, Jumapili iliyopita ikieleza
kuwa walikuwa wakiuzwa kwa bei ya chini na wafanyabiashara wa Soko Kuu
la Kimataifa la Feri, Dar es Salaam.
Akizungumza jana Tabata Bima, Dar es Salaam ambako
samaki hao wamehifadhiwa, Ofisa Uhusiano wa TFDA, Gaudensia Simwanza
alisema mamlaka hiyo ilianza kufanya uchunguzi baada ya kuona taarifa
kwenye gazeti hili ikiwa ni pamoja na kwenda katika Soko la Feri ili
kujua namna wanavyoingizwa nchini.
“Samaki hawa ni wabovu lakini walikuwa wanauzwa
mitaani kwa bei ndogo na tulimkuta mmoja wa wasambazaji akiwa na maboksi
10 ya samaki walioharibika baada ya kumbana ndipo alituelekeza
anapowanunua ikabidi tuje kwa ajili ya kuhakikisha na ndipo tukawakamata
wahusika,” alisema Simwanza.
Alisema bei ya kawaida ya samaki aina ya vibua ni
Sh30,000 mpaka Sh35,000 kwa boksi moja la kilo 10 lakini mfanyabiashara
huyo alikuwa anawauza kwa Sh23,000.
Alisema walipofika katika eneo hilo walikuta
makontena mawili, moja lilikuwa limejaa samaki ambao walionekana kuwa
wazima huku lile lililokuwa nusu lilikuwa na samaki walioharibika
kutokana na kutoa harufu na kuzingirwa na inzi.
Simwanza alisema Kampuni ya Sais Boutique ilipewa
kibali cha kuingiza samaki Julai 8, mwaka huu na kwa mujibu wa taratibu
za TFDA, kila mfanyabiashara mwenye kibali anapoingiza bidhaa anapaswa
aipeleke ikaguliwe kabla ya kuiingiza sokoni ili kujiridhisha kama
inafaa kwa matumizi ya binadamu.
Alisema kampuni hiyo ilikiuka taratibu hizo na
kuanza kuuza samaki hao kabla hawajakaguliwa na kusema kwamba kufanya
hivyo ni kosa kubwa.
Alisema kutokana na kosa hilo, mmiliki wa kampuni
hiyo, Sadick Mapolo yuko chini ya ulinzi akisubiri kuchukuliwa hatua za
kisheria kulingana na kosa alilofanya huku taratibu za kuteketeza bidhaa
hiyo zikifanyika.
Alisema eneo ambalo linatumika kuhifadhia na kuuza samaki hao siyo rasmi kwani halikusajiliwa na TFDA.
“Hapo alipo ana kosa jingine kwani amehifadhi
chakula hiki katika sehemu isiyo salama. Angalia kontena zilizowekwa
samaki hawa zimezungukwa na gereji. Tulivyofika tulihisi kumehifadhiwa
mizigo tu ya kawaida, hatukudhani kama kuna chakula,” alisema Simwanza.
Maofisa wa TFDA walichukua sampuli ya samaki aina
ya Kolekole ambao wametokea Yemen waliopo katika kontena ambalo lilikuwa
halijaanza kuuzwa lenye kilo 27,500 ili kuwapima.
No comments:
Post a Comment