- Yadai ameshindwa kuwakamata watuhumiwa wanaowamwagia tindikali viongozi wa dini.
Dar es Salaam. Tukio la
kumwagiwa tindikali Padri wa Kanisa la Romani Katoliki Parokia ya
Machui, Joseph Mwang’amba huko Zanzibar limechukua sura mpya baada ya
Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC) kumtaka Kamishna wa Polisi
Zanzibar, Mussa Ali Mussa kufukuzwa kazi.
Makamu Rais wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi
aliliambia gazeti hili jana kuwa anapaswa kuondolewa kwa sababu ya
kukithiri kwa matukio hayo visiwani.
Askofu Niwemugizi alisema kamanda huyo anapaswa
kuchukuliwa hatua kwa kuwa ameshindwa kukamata watu wanaofanya vitendo
viovu dhidi ya viongozi wa dini.
Kwa upande wake Kamishna Mussa alisisitiza hawezi
kujiuzulu na kwamba anayestahili kulaumiwa ni Mkurugugenzi wa Mashitaka
(DPP) kwa sababu kwa upande wake alishawakamata watuhumiwa wa matukio
hayo.
“Kazi yangu mimi ni kupeleleza na kukamata
watuhumiwa,ila kazi ya kushitaki watu ni ya DPP hivyo mimi siyo wa
kulaumiwa’Alisema .
Hili ni tukio la nne la uhalifu dhidi ya viongozi
wa dini huko Zanzibar baada ya kuuawa kwa Padri Evarist Mushi wakati
Padri Ambrose Mkenda alipigwa risasi na Katibu wa Mufti, Sheikh Fadhili
Soraga alimwagiwa tindikali.
Katika hatua nyingine, Askofu Niwemugizi alisema
kuwa matukio hayo kwa sasa yamekuwa wazi kwamba ni mpango wa kuangamiza
Ukristo na Wakristo kwa ujumla katika Visiwa vya Zanzibar.
“Uchochezi umefanywa wa kuhamasisha chuki dhidi ya
Ukristo unasikitisha. Tulikaa kama Wakristo tukaiambia Serikali mambo
ambayo inaweza kufanya kukomesha vitendo hivi, lakini hadi sasa hakuna
lililotekelezwa,” alisema na kuongeza:
“Awali ilielezwa kwamba siyo sababu ya kidini,
watu wa Kikundi cha Uamsho ndiyo walioanzisha moto huo na wanauendeleza,
hali inatisha zaidi kwamba hata jamii ya Wazanzibar haionyeshi nia ya
kushiriki kukomesha ukatili huu, kama huyu Padri Mwang’amba amemwagiwa
kwenye kituo cha intaneti ni eneo ambao lina watu mbona mhusika
hajakamatwa? alihoji.
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Kamati ya Haki na
Maadili kwa Jamii kwa Viongozi wa Dini ya Kikristo, Mchungaji William
Mwamalanga alisema kuwa Kamishna huyo wa Polisi anatakiwa kufukuzwa kazi
kwa kuwa anaichafua Zanzibar kwa kushindwa kudhibiti matukio hayo ya
uhalifu kwa makusudi, pia amejaa udini.
No comments:
Post a Comment