Thursday, 1 March 2018

BALOZI SEIF AHAIRISHA MKUTANO WA TISA WA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiahirisha Mkutano wa Tisa wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar katika Majengo ya Baraza hilo yaliopo Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Baadhi ya Mawaziri wa SMZ na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakifuatilia Hotuba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipotoa Hoja ya Kuahirisha Mkutano wa Tisa wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar .
Baadhi ya Manaibu Mawaziri wa SMZ na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakimsikiliza Balozi Seif alipokuwa akisoma Hotuba ya Kuahirisha Mkutano wa Tisa wa Baraza la Tisa la Wawakilishi.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar M,h. Zubeir Ali Maulid akiongozwa na Askari wa Baraza hilo wakitoa nje ya Ukumbi baada kufungwa kwa Mkutano wa Tisa wa Baraza la Tisa la Wawakilishi huko Chukwani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akibadilishana mawazo na Mwakilishi wa Jimbo la Dimani Dr. Mwinyihaji Makame Mwadini baada ya kufungwa kwa Mkutano wa Tisa wa Baraza la Tisa la Wawakilishi.

Picha na – OMPR – ZNZ.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mapambano yake dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa Kijinsia vilivyokithiri katika maeneo mbali mbali Nchini, kamwe haitamvumilia, kumuonea aibu, wala muhali Mtu yeyote wa cheo chochote na ngazi yeyote pindi atakapobainika kuhusika na vitendo hivyo.
Akitoa Hoja ya kuahirisha Mkutano wa Tisa wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa ukifanyika katika Majengo ya Baraza hilo Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alionya na kutahadharisha wazi kwamba Viongozi na Wananchi wanapaswa kutambua kuwa Sheria ni Msumeno.

Balozi Seif alisema Serikali itaendelea kuchukuwa hatua kali za kisheria dhidi ya wote watakaobainika kushiriki katika kadhia hiyo ikiwemo wafanyaji na wale wote wanaoshiriki katika kuwalinda na kuwakingia kifua wahalifu wote wa masuala ya udhalilishaji wa kijinsia.

Alivinasihi vyombo vya ulinzi na usalama kupambana zaidi dhidi ya vitendo hivyo vinavyolitia aibu Taifa sambamba na kuharibu maisha ya Wananchi, huku Jamii ikipaswa kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo hivyo katika Mkakati wa kukabiliana na tatizo hilo baya Kijamii na hata Kidini.

Balozi Seif alisema tabia ya baadhi ya Watu hasa Familia kuzimaliza kesi za Udhalilishaji Majumbani itakupunguza kasi ya Serikali kuwashughulikia wahalifu hao na kuwanasihi Wananchi wahusika kufika Mahakamani kwa kutoa ushahidi utakaotoa nguvu ya sheria kuchukuwa mkondo wake na haki kupatikana ili hatimae kuvimaliza vitendo hivyo katika Taifa hili.

Alieleza kwamba Baraza la Wawakilishi tayari limeshapitisha Sheria ya adhabu kwa wahusika wa vitendo vya udhalilishaji, ambapo imeweka bayana kuwa Mtuhumiwa ye yote wa kosa la udhalilishaji hatopaswa kupewa dhamana.

No comments:

Post a Comment