Wednesday 13 November 2013

Kikwete akataa zawadi ya dhahabu


KATIKA hali ambayo watu wengi wasingetarajia, Rais Jakaya Kikwete amekataa zawadi ya dhahabu aliyopewa na Kampuni ya Nyamigogo Grand Vezir Holdings ya mkoani Geita.
Badala yake ameelekeza dhahabu hiyo safi yenye uzito wa gramu 227 na yenye thamani ya Sh milioni 16 iuzwe na fedha zake zitumike kusaidia watoto yatima.
Rais alitoa maelekezo hayo juzi baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo wakati wa sherehe ya kuzindua mgodi wa uchenjuaji dhahabu wa kampuni hiyo, nje kidogo ya mji mdogo wa Kharuma yaliko makao makuu ya wilaya mpya ya Nyang’hwale, Geita.
Baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo, Rais Kikwete aliuliza: “Sasa nifanye nini na zawadi hii? Nawarudishieni hii dhahabu, iuzeni popote mnakotaka na fedha itakayopatikana tutawapa watoto yatima.”
Akizungumza na wananchi katika mgodi huo, Rais Kikwete aliupongeza uongozi wa mgodi huo akisema umeongeza thamani ya dhahabu na ya maisha ya wananchi katika eneo hilo nje ya mji huo.
Hata hivyo, Rais aliushauri uongozi wa mgodi huo kufanya jitihada za kuboresha teknolojia inayotumika.
“Mmefanya vizuri sana na mgodi huu ni mradi wa maana sana kwa kuongeza thamani ya dhahabu na kuboresha maisha ya wananchi katika eneo hili. Ubunifu huu unastahili pongezi.”
Aliongeza: “Lakini lazima tuboreshe teknolojia. Teknolojia inayotumika kwenye mgodi huu bado ni ya zamani kidogo. Hii ni sawa na hadithi ya mtu mwenye chongo katika jamii ya vipofu watupu. Yeye anaonekana kama mfalme.”
Mgodi wa Nyamigogo ambao ni wa marudio kwa maana ya kuzalisha dhahabu kutokana na mchanga ambao huko nyuma ulifukuliwa na kutoa dhahabu, ulianzishwa mwaka 2011 na mpaka sasa zimewekezwa Sh bilioni 1.6 katika uendelezaji wa mgodi huo.
Risala ya uongozi wa mgodi ilisema mgodi huo unaozalisha kiasi cha gramu kati ya 500 na 600 kwa mwezi unaajiri watu 45 wakiwamo wanawake 10.
Tangu kuanzishwa kwake, mgodi umekuwa unaunga mkono shughuli za jamii inayouzunguka, ikiwa ni pamoja na kujenga zahanati na madarasa ya shule katika vijiji viwili.
Rais Kikwete alizindua mgodi huo, ikiwa ni sehemu ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika ziara yake rasmi ya kikazi katika mkoa wa Geita, moja ya mikoa minne ambayo aliianzisha mwaka jana. Mingine ni Simiyu, Njombe na Katavi.

No comments:

Post a Comment