Wednesday, 5 February 2014

MIEZI 9 BAADA YA WEMA KUMLIPIA MILLION 13 KAJALA AIBUKA TAJIRI GHAFLA MIEZI

MIEZI tisa baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar kumhukumu staa wa filambu za Bongo, Kajala Masanja kifungo cha miaka mitatu jela au faini ya shilingi milioni 13 kwa kosa la utakatishaji fedha na Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu kumlipia hivyo kuwa huru, hali ya maisha ya msanii huyo imebadilika ghafla na sasa ameibuka katika utajiri wenye maswali na majibu.
Kajala Masanja.
Chanzo makini kimeliambia gazeti hili kwamba, Kajala ambaye alitoka mahabusu ya Segerea jijini Dar, Machi 25, 2013 akiwa hana mbele wala nyuma kiasi cha kutia huruma, sasa anazikamata za kutosha kiasi cha watu wake wa karibu kumshangaa.
MANUNUZI YAKE
Chanzo kimebainisha kuwa, Kajala ameagiza kutoka China kontena lenye urefu wa futi 20 likiwa limesheheni  samani za ndani. Samani za ndani ni fenicha mbalimbali.

“Hivi mnajua kwamba Kajala yuko juu. Naweza kusema ni tajiri kwa sasa, maisha yake ni poa. Hivi ninavyoongea kuna kontena la futi arobaini linakuja Dar, ndani mna samani tu,” kilisema chanzo hicho.
AMWAGA MILIONI 90 KUTENGENEZA FILAMU
Katika hali inayoendelea kutafsiriwa kuwa ni kuzidi kuonesha ukwasi alionao, msanii huyo ameshatumia shilingi milioni 90 kwa ajili ya kutengeneza filamu zake tatu, kila moja ikitumia bajeti ya milioni 30 za Kibongo.

Filamu ya Kajala ambayo iko njiani kutoka inaitwa Laana. Inadaiwa mpango wake ni kutengeneza filamu 10 ambazo atakuwa akiziuza kwa nyodo. Kama ni hivyo atatumia shilingi milioni 300 kwa filamu hizo kumi.
ATUMIA MILIONI 11 KUNUNUA VITO VYA THAMANI
Mbali na kuvaa magauni na viatu vya bei mbaya, hivi karibu staa huyo alitua Dar akitokea China ambapo alipigilia vito vya gharama ya maisha ya familia nzima.

“Juzikati Kajala katoka China na cheni ya dhahabu kainunua dola za Marekani elfu tatu, bangiri pia ya dhahabu ya dola elfu mbili na mia tano na hereni za gold (dhahabu) za dola elfu moja mia tano,” kilisema chanzo.
Kwa mahesabu ya sasa, kiasi hicho cha dola kikibadilishwa na shilingi ya Tanzania, Kajala alitumia kama milioni 11 kununua vito hivyo tu. 
ANAYEMPA JEURI ATAJWA
Inadaiwa mcheza filamu huyo amekuwa akipata jeuri hiyo kutoka kwa mwanaume bilionea wa Ghana aliyejulikana kwa jina moja la Safara ambaye walikutana nchini China. Inadaiwa Safara anaishi Marekani lakini ndiye anayeshika tenda ya kuinunulia serikali ya Ghana vitu mbalimbali.

MWISHO DESEMBA KUISHI NYUMBA YA KUPANGA
Habari zikazidi kumiminika kwamba, Safara amemwambia Kajala mwisho Desemba mwaka huu kuishi kwenye nyumba ya kupanga, mwakani mjengo wake utakuwa umekamilika.

Hata hivyo, haijaelezwa kama ameshapata kiwanja cha kujengea au la! Ingawa habari zinasema nyumba anayoishi sasa Kajala imeshalipiwa kodi ya mwaka mmoja na tajiri huyo wa Ghana.

AMFADHILI WEMA

Ikazidi kudaiwa kuwa, katika ziara ya baadhi ya mastaa jijini Arusha hivi karibuni wakiongozwa na Wema ambako kulikuwa na shoo ya muziki wa Kizazi Kipya, Kajala alimsaidia Wema mambo mbalimbali zikiwemo pesa ili kufanikisha shughuli hiyo iliyohitaji umakini wa hali ya juu.
“Mbali na fedha hizo, Kajala wa zamani si huyu wa sasa, ila ninashomsifu bado anamheshimu sana Wema, anajua ndiye amechangia mafanikio yake, kama siku zile asingetoa zile milioni kumi na tatu Kajala angekuwa gerezani,” kilisema chanzo hicho.
ALIPOTOKA GEREZANI
Inadaiwa baada ya kutoka Segerea, Kajala aliishi maisha ya kuwa na shida hata shilingi elfu kumi ilimsumbua, Wema ndiye aliyekuwa akimbeba kwa vijisenti vya matumizi na baadaye alimwajiri kwenye kampuni yake ya filamu ya Endless Fame kama sekretari. Kampuni hiyo kwa sasa imesimama.

HUENDA CHINA KINYEMELA?
Baada ya kuona safari zake zimezaa matunda na kuhisi watu wanafuatilia nyendo zake, likiwemo gazeti hili, Kajala ambaye husafiri mara kwa mara, amekuwa akidai anakwenda Zanzibar licha ya hati zake za kusafiria kuoneshwa zimegongwa mihuri ya China na Dubai.

KAJALA SASA
Alipoulizwa kwa njia ya simu juzi kuhusiana na ukwasi wake kwa sasa, Kajala alisema anachojua yeye anaishi maisha ya kawaida, tafsiri kwamba amekuwa tajiri ghafla inafanywa na watu  wanaomuona.

“Mimi naishi kawaida tu, huo utajiri wanauona wao. Unajua haya ni maisha, leo unakuwa hivi, kesho unakuwa vile ndicho ninachoweza kukisema, siwezi kusimulia kila kitu,” Alisema kajala

KIAMA CHA BIASHARA YA NGONO..MASHOGA NA MACHANGU IRINGA....!SOMA ZAIDI HAPA.....!

SERIKALI ya Mkoa wa Iringa imeagiza  kukamatwa kwa wanawake wanaouza miili (ukahaba) na wanaume mashoga kama inavyofanywa na Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM,’ ya Global Publishers.

Agizo hilo limetolewa hivi karibuni katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika Ukumbi wa Siasa ni Kilimo chini ya mkuu wa mkoa huo, Christine Ishengoma. 

Hayo yamekuja baada ya Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa, Amani Mwamwindi kuwaeleza wajumbe kuwa mbali ya kusikia kutoka majiji kama Dar na mengine nchini kwamba biashara za ukahaba na ushoga ziko juu, uchunguzi unaonesha mji wa Iringa ni miongoni mwa miji ambayo biashara hiyo inaendelea kukua kwa kasi. 

“Ndugu  wajumbe, Manispaa ya Iringa ina watu wanaofanya biashara ya ushoga na ukahaba. Mimi meya nina ushahidi  wa kutosha. Idara inayohusika na vita dhidi ya Ukimwi katika halmashauri ya manispaa inaujua mtandao mzima wa biashara hiyo haramu,” alisema meya huyo. 

Kufuatia ushahidi huo kutoka kwa meya, mkuu huyo wa mkoa alilazimika kusimama na kuwataka wahusika kuwakamata watu hao wote ili ikibidi wasaidiwe kupewa miradi rafiki badala ya kuendelea na biashara hiyo haramu.

KILO 201 ZA MADAWA YA KULEVYA ZILIZOKAMATWA JANA BAHARI YA HINDI HIZI HAPA


  Polisi wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya wakifungua dawa zilizokamatwa jana kwenye jahazi liitwalo Kunarak-Iran lililokutwa katika Bahari ya Hindi eneo la Tanzania likiwa na kilo 201 za heroini, pamoja na raia wanane wa Iran na  Wapakistan wanne. 

Kikosi kazi cha Jeshi la Polisi cha Kudhibiti Uharamia Baharini kimekamata kilo 201 za dawa za kulevya aina heroini zilizokuwa zikiingizwa nchini kutoka Iran.
Kamishna wa Polisi, Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, alisema jana kikosi hicho kikiwa kwenye doria ya kawaida kiliona boti ambayo haikuwa na bendera wala kiashiria chochote ndipo walipoitilia shaka na kuamua kuifuatilia.
Nzowa alisema kuwa mzigo huo ni mkubwa zaidi wa heroin kuwahi kukamatwa na vikosi vya doria vya Tanzania. Alisema mara ya mwisho kwa mzigo mkubwa zaidi wa heroin kuwahi kukamatwa ilikuwa mwaka 2012 wakati zilipokamatwa kilo 70 za dawa hizo jijini Dar es Salaam.
Nzowa alisema Kikosi cha Wanamaji kiliposhuku boti hiyo, kiliisimamisha na kugundua kuwa ilikuwa na watu 12. Alisema baada ya uchunguzi wao waligundua kuwa kulikuwa na raia wanane wa Iran na wanne wa Pakistan. “Boti hiyo ilivutwa hadi ufukweni ambako leo (jana) ilifanyiwa uchunguzi na ndipo zikakutwa na kilo 201 za heroin,” alisema Nzowa.
Nzowa alisema boti hiyo iliyosajiliwa Kunarak, Iran, ilikuwa inaongozwa na nahodha mwenye uraia wa nchi hiyo, Ayub Hot (50). Nzowa alisema kitakachofuata sasa ni kufanya upelelezi na kujua walikuwa wanataka kupeleka wapi mzigo huo, kufahamu mtandao wao na walipanga kufanya nini katika ufukwe wa Dar es Salaam.  Alisema baada ya upelelezi wao kukamilika watu hao watafikishwa mahakamani. Naye Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Polisi, ACP Mboje Kanga alisema watu hao 12 hivi sasa wamewekwa mahabusu ya wanamaji na kikosi hicho kwa kushirikiana na Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya wataendelea na upelelezi.
Taarifa ya mwaka 2011 ya Kitengo cha Dawa za Kulevya iliyochapishwa katika ripoti ya Kitengo cha Dawa za Kulevya cha Marekani inaeleza kuwa, heroini huingia Tanzania kupitia Bahari ya Hindi ikitokea Afghanistan, Iran, Pakistan na Falme za Kiarabu.

Tuesday, 4 February 2014

RAIS KIKWETE AKUTANA NA MHIFADHI WA SOKWE DKT. JANE GOODDALL IKULU DAR



Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimsikiliza mhifadhi wa Sokwe wa kimataifa Dkt.Jane Goodall wakati mhifadhi huyo alipomtembelea Rais Ikulu na kumwelezea kazi zake mbalimbali za uhifadhi nchini. Dkt.Goodall anajihusisha na uhifadhi wa Sokwe katika hifadhi ya Gombe mkoani Kigoma na kazi yake imeipatia Tanzania umaarufu mkubwa Duniani.
Dkt. Goodall ni mwanzilishi wa taasisi ya Jane Goodall Institute inayojihusisha na uhifadhi wa Sokwe.


Monday, 3 February 2014

MALI YA HAYATI MANDELA YATANGAZWA

Mandela alifariki mwezi Disemba mwaka jana akiwa na umri wa miaka 95
Hayati Nelson Mandela, aliachia familia yake mali yake yenye thamani ya dola milioni 4.1.
Sehemu ya mali hiyo pia itatolewa kwa chama tawala ANC, wafanyakazi wake wa zamani na shule kadhaa ambako alisomea.
Hayo ndio yalikuwa mapenzi ya Mandela ambayo yalikuwa kwenye wasia wake uliosomwa hadharani kwa familia nzima.
Jaji wa mahakama ya juu zaidi nchini Afrika Kusini Dikgang Moseneke aliyekabidhiwa jukumu la kusoma wasia huo wenye kurasa 40 na kuhakikisha unatekelezwa ,alisema hapajakuwa na pingamizi zozote kuhusu yaliyomo kutoka kwa familia ya Mandela.
Jaji alisema kuwa baadhi ya mali hiyo itagawanywa katika wakfu tatu za Mandela ikiwemo moja ya familia yake ambayo itawafadhili zaidi ya watoto na wajukuu 30 wa Mandela pamoja na vitukuu wake.
Wafanyakazi wa karibu wa Mandela watapata randi 50,000 kila mmoja. Shule ambazo Mandela alisomea zitapata randi laki moja kila shule.
Hayati Mandela alifariki akiwa na umri wa miaka 95.
Familia ya Mandela tangu hapo imekuwa ikizozana kuhusu urithi wa hayati Mandela na kuna hofu kuwa huenda wasia huu ukasababisha mgogoro mwingine kuhusu mali hiyo.
Mali ya hayati Mandela inajumuisha nyumba na hakimiliki za vitabu ikiwemo kimoja kuhusu maisha yake kwa jina ''Long walk to freedom''
Baadhi ya mali nyingine za hayati Mandela ni nyumba ya kifahari mjini Johannesburg na nyumba nyingine katika kijiji alikozaliwa Eastern Cape.

RAIS KIKWETE ATEMBELEA KUKAGUA MAJENGO YA BUNGE DODOMA KUELEKEA BUNGE LA KATIBA


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikagua sehemu ya Siti za kukaa ndani ya ukumbi wa Bunge mjijini Dodoma wakati alipotembelea na kukagua kampuni inayokarabati na kufanya marekebisho kwa ajili ya kupokea wajumbe wa Bunge la katiba linalotarajia kuanza baadaye mwezi huu.
 Rais Jakaya Kikwete, akijaribu kipaza sauti katika moja ya siti za ukumbi huo.
 Muonekano wa siti za ukumbini humo baada ya marekebisho...
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitembezwa sehemu mbalimbali za majengo ya Bunge mjijini Dodoma alipotembelea kukagua maendeleo ya ukarabati na marekebisho ya ukumbi wa Bunge kujiandaa na Bunge la Katiba marekebisho  tayari kwa kupokea wajumbe wa Bunge la katiba baadaye mwezi huu.


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa kampuni ya ujenzi inayokarabati na kufanyia marekebisho ukumbi wa bunge mjini Dodoma tayari kwa kupokea wajumbe wa Bunge la katiba baadaye mwezi huu.

Sunday, 2 February 2014

MWENYEKITI WA CCM, RAIS KIKWETE AONGOZA SHEREHE ZA MIAKA 37 ZA CCM LEO MJINI MBEYA


RAIS JAKAYA KIKWETE AGUSWA NA UTENDAJI WA KINANA, ATAKA AWE MFANO WA KUIGWA

Kikwete akizungumza kwenye kilele cha miaka 37 ya CCM leo









MWENYEKITI wa CCM, Rais Jakaya Kikwete leo amevunja ukimya na kuzungumzia suala la mawaziri waliotuhumiwa na wananchi kuwa mizigo wakati wa ziara za Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na baadhi ya wajumbe wa sekretarieti katika mikoa kadhaa nchini mwishoni mwa mwaka jana.
 
"Najua wapo baadhi ya watanzania, walitaka Mawaziri waliotajwa kuwa ni mizigo wafukuzwe kazi, na kwa vile halikufanyika basi suala hilo limegeuzwa kuwa la malumbano,  ni vyema ieleweke kuwa kuitwa kwa Mawaziri hao na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hakuna maana ya kuishia kufukuzwa", alisema, Kikwete leo akihutubia maelfu ya watu katika sherehe za kilele cha miaka 37 ya CCM, kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya. 

Alisema Mawaziri hao waliitwa kwa sababu ya kuwepo matatizo yaliyoonekana yanatakiwa yapatiwe ufumbuzi, matatizo hayo yamezungumzwa na maelekezo kutolewa kuhusu cha kufanya.

"Kamati Kuu ya CCM imetimiza wajibu wake uliobaki ni wa serikali.Kamati Kuu itaendelea kufuatilia na kama hakuna maendeleo ndipo inapoweza kuamua kuomba mamlaka ya uteuzi ichukue hatua zipasazo dhidi ya mhusika.Huko hatujafika" alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alimpongeza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, akisema, ziara ambazo amekuwa akifanya ni mfano unaopaswa kuigwa na viongozi wengine hasa wa CCM kwa sababu ndio hasa unaotakiwa.

Alisema ziara za Kinana zinakijenga Chama na kutoa taswira nzuri ya CCM katika jamii kwani zinahuisha uhai wa CCM kwa kuwa Katibu Mkuu huyo katika ziara hizo huenda hadi kwa wanachama waliopo ngazi za chini.

"Katibu Mkuu Kinana amekuwa anafanya mambo ambayo baadhi ya watu wanadhani kuwa ni mageni, lakini katika kufanya hayo amekuwa pia akionyesha umahiri na ujasiri mkubwa kwa kwenda  maeneo ambayo ni magumu kufikika" alisema Rais Kikwete na kuongeza;

"Katika ziara hizo  wakati mwingine amekuwa anatumia njia za usafiri zinazoogopesha, amewahi kutumia meli  ya MV Songea kutoka mkoani Ruvuma hadi Mbeya, amepanda milima na mabonde kwa magari katika maeneo ambayo ni hatari, lakini lengo likiwa ni kuhakikisha anawafikia wanachama wa ngazi za chini kabisa".

Rais Kikwete alisema mambo mengine yalivyomvutia katika ziara za Kinana, ni hatua ya Katibu mkuu huyo kwenda kukaa na  kula na wananchi katika ngazi za chini na kisha kufanya nao kazi za maendeleo  na zaidi kutoa fursa kwa wananchi kueleza matatizo na manung'uniko yanayowasibu.

Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa alisema Katibu mkuu wa Chama amekuwa anashiriki katika kutafuta majawabu na matatizo anayoambiwa hali ambayo imesaidia sana kumaliza baadhi ya matatizo kulekule mikoani.

"Pale ambapo pamekuwa panahitaji hatua zaidi za serikali hakusita kutoa taarifa kwa Waziri Mkuu, vile vile amekuwa anatoa taarifa ya ziara zake kwenye Kamati Kuu ya CCM" alisema Rais Kikwete.

AJALI MBAYA YATOKEA MAENEO YA MZUNGUKO( ROUND ABOUT) YA KWENDA BARABARA YA KYAKA- MTUKULA JIONI YA LEO BUKOBA

 Lori kubwa limepata ajali mbaya maeneo ya mzunguko, Barabara ya kuelekea Kyaka jioni ya leo, ni magari matatu yaliyokuwa yamefuatana yakielekea nchini Uganga yakiwa yamepakia makaa ya mawe kwa mujibu wa maelezo ya awali,chanzo cha ajali inasemekana gari moja wapo lilikatika breki,Habari kamili hazijasibitishwa kuhusiana na chanzo cha ajari,Magari yanaonyesha ni  ya nchini zambia
 Majawapo ya gari liliokuwa kwenye msafara
 Askari wa usalama barabarani wakiwa katika tukio la ajali
 Hii ndio hali halisi ya injini
 Wananchi wakishuhudia tukio
 Ni baadhi ya mifuko inayosemekana ni makaa ya mawe
 Mmoja wa madereva wa malori hayo ya Malawi
 Inasemekana ni makaa ya mawe yaliyokuwa yanapelekwa Uganda
Ni mojawapo ya namba ya gari iliyopata ajali