
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Nnauye akisalimiana na Viongozi mbalimbali kwenye Ofisi za Mkuu wa Mkoa leo

Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye leo tarehe 14 April, 2016 akiwa mkoani Kagera ahaidi kuihamishia Wizara yake kwenye mikoa na Halmashauri za Wilaya kwa wadau wanaohusika ili kurasmisha shughuli na majukumu ya wizara hiyo ili iweze kupata ufanisi.
Akiongea na wadau mbalimbali wanaohusika na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alisema kuwa lengo la ziara yake ni kuja mikoani kujionea changamoto mbalimbali za wizara yake ili aweze kuzifanyia kazi kwa kuishusha wizara kwa wadau wanaohusika ili kutekeleza majukumu yake.
Katika kikao hicho Waziri Nape alisema kuwa sekta nne ambazo ni Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo zimekuwa hazifanyi kazi zake vizuri kutokana na watendaji wake kutokuwa na idara au vitengo vinavyohusika moja kwa moja na kazi zao jambao ambalo linawafanya kujishikiza katika sehemu au idara nyingine.




Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Nnauye akisikilizwa kwa makini na Wadau wa Maendeleo hapa Bukoba, Picha na Faustine Ruta, Bukoba






Sekta ya Habari
Mhe, Nape aliagiza Halmashauri za Wilaya kuajiri Maafisa Habari katika Halmashauri ambazo hazina Maafisa hao, pili kuwaruhusu Maafisa hao kuingia kwenye vikao vyote vya maamuzi ili kuweza kuzisemea taasisi hizo. Na kutenga bajeti kwa Maafisa habari hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu.
Kuhusu changamoto ya vitendea kazi Mhe. Nape alisema kuwa Wizara yake imeanza kuwajibika kwa kuto IPad za kisasa kwa Maafisa Habari waliopo Mikoani na katika Halmashauri za Wilaya ili ziweze kuwasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha, kwa mkoa wa Kagera alitoa Ipad tano kwa Maafisa habari.

Aidha, Mhe. Nape aliwahakikishia Waandishi wa Habari kuwa maslahi yao yataboreshwa chini ya usimamizi wake kama Waziri mwenye dhamana ambapo alisema kuwa Serikali ipo kwenye mchakato wa kukamilisha Mswada wa huduma kwa vyombo vya habari ambao utazingatia mahitaji na maslahi ya waandishi wa habari.















Sekta ya Michezo
Katika sekta ya Michezo Mhe, Nape aliwakumbusha Makatibu Tawala wa Mikoa wao kama Wenyeviti wa kamati za michezo za mikoa kutembelea na kukaa na viongozi wa vyama vya michezo kuwakumbusha majukumu yao na kupitia mara kwa mara mipango kazi yao ya kazi aidha, kusimamia upatikanaji wa viongozi wenye wajibu katika michezo na siyo vibarua wa kuingia kuwatumikia baadhi ya watu Fulani.
Aidha, alimuagiza Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba na Wenyeviti wa Halmashauri kuhakikisha wanasimamia urudishwaji wa viwanja vilivyoporwa na kutopitisha ramani za mipango miji zisizozingatia utengwaji wa maeneo ya wazi ya michhezo.
Sanaa
Mhe. Nape alisema kuwa Serikali inakusudia kuirasmisha sanaa kuwa shughuli za uchumi badala ya kuwa shughuli za burudani tu kwasababu kwasasa sanaa inaonekana kuwa ni kuburudisha tu wakati imekuwa ikitoa ajira kwa vijana wengi. Aidha, Serikali inakusudia kuwasimamia wasanii kuondokana na matapeli wanaonufaika kupitia kazi zao nao kubaki hoi hae.
Katika Sekta ya Utamaduni Mhe, Nape alisema Serikali inakusudia kutumia utamaduni kama nyenzo ya utalii katika taifa la Tanzania
Ili kutatua changamoto zinazoikabili Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo zilizopo katika mikoa na Halmashauri za Wilaya Mhe. Nape alisema Wizara yake imeanza kufanya mazungumzo na Ofisi ya Rais TAMISEMi ili kuanzisha vitengo au idara katika Mikoa na Halmashauri za Wilaya.
Baada ya kuongera na wadau Mhe. Nape alitembelea Uwanja wa Kaitaba na kujionea maendeleo ya ukarabati wa uwanja huo ambapo amewahakikishia wadau wa michezo wa Mkoa wa Kagera kuwa atahakikisha anamsukuma mkandarasi ili akamilishe uwanja huo mapema iwezekanavyo.
